CURRENT NEWS

Thursday, March 23, 2017

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE IMEITAKA SERIKALI KUHAKIKISHA INATOA FEDHA ZA MRADI WA UJENZI WA JENGO LA ABIRIA NAMBA TATU

KAMATI ya Kudumu ya Bunge imeitaka serikali kuhakikisha inatoa fedha za mradi wa ujenzi wa jengo la abiria namba tatu (terminal III) kwa wakati ili mradi huo uweze kukamilika kama ilivyopangwa. 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Norman Sigalla aliyasema hayo wakati wa kufanya majumuisho baada ya kutembelea mradi huo leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). 

Alisema kukamilika kwa jengo hilo kwa wakati uliopangwa utawapa heshima Watanzania lakini pia kupunguza msongamano katika jengo la sasa la Terminal II. 

“Nchi inapoenda kwa sasa ni kuzuri, lakini ili kukamilika ujenzi huu kwa wakati tunaomba serikali itoe fedha ili kufanikisha hilo, baada ya kukamilika kila ndege itatua hapa nchini na hivyo kuongeza pato la Taifa,” alisema Profesa Sigalla. 

Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Salim Msangi alisema, miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa mradi huo ni serikali kutotoa fedha kwa wakati pamoja na sheria ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ilipitishwa mwaka 2015. 

Alisema kabla ya sheria hiyo wakati inapitishwa vifaa vya ujenzi wa uwanja huo vilikuwa na msamaha wa kodi lakini baada ya kupitishwa msamahaka huo uliondolewa hali iliyosababisha baadhi ya vifaa kukwama bandarini na wakati mwingine kukaa muda mrefu. 

Aliongeza kuwa mradi huo ulikuwa unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka jana lakini ulichelewa kutokana na kuchelewa kuwasilishwa kwa fedha zaidi ya Sh bilioni 290 kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo. 

“Tunaiomba serikali iwezeshe kupatikana kwa fedha za mradi kwa wakati pamoja na kutatua changamoto zinazojitokeza ili kutochelewesha mradi na kuepuka gharama zinazoweza kujitokeza kutokana na kuchelewa kukamilika kwake,” alisema. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamuliho alitoa ufafanuzi kuhusu notisi iliyotolewa na Mhandisi Mshauri ya kusitisha huduma kuanzia jana hadi atakapoliwa deni lake. 

Alisema tayari serikali inafanyia kazi deni hilo na kwamba ipo katika hatua nzuri ya kuhakiki vocha za malipo kabla ya kufanya malipo ya mhandisi huyo. 
01.Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Miundombinu Mhe.Prof Norman Sigalla akizungumza na wana kamati wakati wa ziara ya mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abria (terminal) katika kiwanja cha ndege cha kimataifa Julius Nyerere leo jijjini Dar es Salaam. 
02.Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamriho akizungumza wana kamati wakati wa ziara ya mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abria (terminal) katika kiwanja cha ndege cha kimataifa Julius Nyerere leo jijjini Dar es Salaam. 
03.Mbunge wa Jimbo la Kwimba,Shanif Mansoor akifafanua jambo leo jijini Dar es Salaam.
Wana kamati wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Miundombinu wakimsikiliza Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Miundombinu Mhe.Prof Norman Sigalla
.Wana kamati wa kamati ya kudumu ya Bunge wakitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abria (terminal) katika kiwanja cha ndege cha kimataifa Julius Nyerere leo jijjini Dar es Salaam. 
Ujenzi ukiendelea wa jengo la abiria namba tatu (Terminal. )Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania