CURRENT NEWS

Saturday, March 25, 2017

LUKOA-VIWAVIJESHI WANAOSHAMBULIA MAZAO WAENDELEA KUANGAMIZWA CHALINZE

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Edes Lukoa akizungumza. 

Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete akizungumza na madiwani wa halmashauri hiyo katika baraza la madiwani. (picha na Mwamvua Mwinyi)


Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
HALMASHAURI ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, imefanikiwa kudhibiti wadudu aina ya viwavijeshi wanaoharibu mazao mbalimbali ambapo waliingia katika baadhi ya maeneo mwanzoni mwa mwezi huu.
Aidha wakulima katika halmashauri hiyo wameombwa kuwa wakitoa taarifa mapema mara wanapobaini wadudu hao kushambulia mazao yao.
Akizungumzia kuhusiana na hali ilivyokuwa na namna walivyochukua hatua, Mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze, Edes Lukoa aliipongeza serikali kwa hatua zilizochukuliwa.
Alisema wadudu hao waliingia katika mashamba ya wakulima kuanzia mwanzo wa mwezi wa tatu 2017.
Lukoa alitaja maeneo yaliyokubwa na changomoto hiyo kuwa ni Msoga, Talawanda, Mkange, Vigwaza, Msata, Kibindu, Kiwangwa ambako baada ya kutoa taarifa wataalamu walikwenda na kuangamiza vidudu hivyo.
"Tunashukuru wakati taarifa hizo zinatolewa tayari tulikuwa na chupa 51 zilizoangamiza viwavijeshi katika hekari 3,500"alisema.
Hata hivyo baadhi ya madiwani walishukuru kwa hatua zilizochukuliwa kusaidia wakulima lakini wameomba ziongezwe dawa nyingine ili kumaliza kero hiyo katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu.
Kufuatia hoja hiyo, Lukoa alielezea kwamba tayari halmashauri hiyo imepokea chupa 100 za sumu ya kuangamiza maeneo yaliyobakia.
Alisema anauhakika chupa zilizoongezeka zitamaliza kabisa adha hiyo kwa wakulima.
Nae afisa kilimo wa Halmashauri ya Chalinze, Seth Mgonja alisema ipo mikakati waliojiwekea kudhibiti kero hiyo mara itakaojitokeza wakati mwingine.
Mgonja alisema wametoa maelekezo kwa wakulima kutoa taarifa haraka wakishaona wadudu hao na kuchimba mashimo makubwa endapo wakibaini kuingia kwenye maeneo yao.
Viwavijeshi ni watoto wa vipepeo na kabla ya kukua huwa wakila mazao wakati wa hatua ya lava .
Wadudu hao hula na kumaliza hata shina zima la zao na wanatabia ya kuhama hama.
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania