CURRENT NEWS

Tuesday, March 28, 2017

MAFUNZO YA UFUNGAJI MIGODI YATOLEWA KWA KAMATI YA KITAIFA YA UFUNGAJI MIGODI.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt. Juliana Pallangyo  ( kulia) na Mkuu wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Canada, Sue Steffen,(kushoto) akizungumza wakati wa mafunzo ya kufunga wa migodi yanayotolewa kwa Kamati ya Kitaifa ya ufungaji Migodi.Mafunzo hayo ya siku tano  yanatolewa na Serikali ya  Canada jijini Dar Es Salaam.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt. Juliana Pallangyo  ( katika waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Kitaifa ya ufungaji Migodi  wakati wa mafunzo ya ufungaji wa migodi yanayotolewa kwa siku tano jijini Dar es salaam na Serikali ya Canada. Kushoto kwake ni Mkuu wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Canada, Sue Steffen, na kulia kwake ni Afisa Rasilimali Watu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Suzan Kiwelu.
 Washiriki wa mafunzo ya ufungaji migodi ambao ni Kamati ya Kitaifa ya ufungaji Migodi wakifatilia mada mbalimbali wakati wa mafunzo hayo yanayotolewa kwa siku tano jijini Dar es salaam na Serikali ya Canada.
 Afisa Rasilimali Watu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Suzan Kiwelu ( kulia) na Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija( kushoto) wakifuatilia mada wakati wa mafunzo hayo yanayotolewa kwa siku tano jijini Dar es salaam na Serikali ya Canada.
Wakufunzi wa mafunzo ya ufungaji migodi kutoka nchini Canada wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt. Juliana Pallangyo ( hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo. 
Na Zuena Msuya DSM,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Juliana Pallangyo amefungua mafunzo ya ufungaji wa migodi yanayotolewa kwa wataalam wa mbalimbali wanaoshiriki katika Kamati ya Kitaifa ya ufungaji wa  Migodi.
Watalaam hao wanatoka katika Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wa ufungaji wa migodi nchini.Mafunzo hayo yanatolewa jijini Dar Es Salaam,na Serikali ya Canada kwa siku tano kuanzia 27-31 machi 2017.
Akizungumza wakati wa akifungua wa mafunzo hayo, Dkt. Pallangyo alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wataalamu wa migodi nchini kuwa na uelewa zaidi juu ya hatua zote zinazotakiwa kufuatwa wakati na baada ya ufungaji wa migodi ili kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza  baada ya migodi kufungwa.
Dkt. Pallangyo, alifafanua kuwa, kwakuwa Serikali ya Canada imejikita katika Sekta ya Madini kwa zaidi ya miaka 200, hivyo  mafunzo hayo yatawasaidia wataalam wa ndani kufahamu na kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza  kupitia migodi iliyokwishafungwa katika nchi hiyo ili yasijitokeze hapa nchini.
" Tusiwe watu wa kusoma tu na kufunga migodi, tujifunze kwa vitendo kutoka kwao makosa waliofanya wakati wa ufungaji wa migodi kwa kuwa Canada ipo katika Sekta ya madini kwa zaidi ya miaka 200 na tujirekebishe, ili makosa yaliyotokea kwa yasijirudie katika migodi yetu," alisisitiza Dkt.Pallangyo.
Vilevile,  ameiomba Serikali ya Canada kutoa mafunzo hayo mara kwa mara na kwa muda mrefu ili kupata wataalam wengi zaidi na wenye uelewa mpana katika Sekta ya Madini hasa ufungaji wa migodi hapa nchini: Mafunzo hayo yatawawezesha watalaam kubaini kodi halisi inachotakiwa kulipwa Serikalini pamoja na njia rahisi ya utunzaji wa ardhi na mazingira kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Canada, Sue Steffen aliesema kuwa nchi yake inauzoefu wa zaidi ya miaka 200 katika sekta ya madini, hivyo wameona ni busara kutoa mafunzo hayo kwa nchi zinazoendelea na zinazochimba madini mbalimbali.
Alisema, lengo ni kutoa elimu na kuzijengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizowahi kujitokeza katika ufungaji wa migodi nchini Canada, na hivyo kuziepusha nchi hizo katika madhara yanayoweza kujitokeza.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Mhandisi Elizabert Nkini alisema kuwa mafunzo hayo yatawaongezea uelewa zaidi katika ufungaji wa migodi, licha kuwepo kwa vigezo vya ufungaji wa migodi hiyo lakini uelewa umekuwa ni mdogo kutokana kutofahamu kwa vitendo changamoto nyingi.
"Migodi nchini ni muhimili mkubwa wa mapato, lakini pia ni chanzo kikubwa cha uharibu wa mazingira, hivyo kama  mazingira na ardhi yetu havitatunzwa vizuri kabla na baada ya kuchimbwa tutaicha nchi yetu katika hali ya jangwa isiyofaa na vyanzo vya maji vitaharibiwa, hivyo mafunzo hayo yatatuwekea utatatibu mzuri wa kuacha mazingira yetu yakiwa salama na ardhi salama pia,". alisema Mhandisi Nkini.
Aidha alisema kuwa elimu hiyo waliyoipata wataifikisha kwa wananchi wanaozunguka Migodi husika ili na wao wawe na uelewa juu ya ufungaji wa migodi kwa kufahamu taratibu na hatua mbalimbali za kufuata kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania