CURRENT NEWS

Thursday, March 23, 2017

MAGARI ZAIDI YA SABA YATEKWA NA MAJAMBAZI HUKO MCHUKWI RUFIJI


Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
Magari zaidi ya saba ya abiria yametekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi huko barabara kutoka Dar es salaam kwenda mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara eneo la Mchukwi .
Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Onesmo Lyanga alisema tukio hilo limetokea usiku wa march 22 kuamkia march 23 mwaka huu.
Akielezea tukio hilo, alisema kwamba watu hao waliweka magogo katikati ya barabara ili kufanya wizi kwa abiria mbalimbali waliokuwemo kwenye magari hayo.
Kamanda Lyanga alisema, baada ya magari kusimama waliwashurutisha abiria kwa kuwapiga kwa mapanga na marungu na kusababisha baadhi yao kujeruhiwa.
"Wameibiwa mali na fedha zao na baadhi yao kujeruhiwa kwa kupigwa "alisema .
Alibainisha kwamba, waliojeruhiwa walifikishwa Kituo cha afya Mchukwi kupata matibabu na kuruhusiwa.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, kwasasa wanawasaka wale wote waliohusika na tukio hilo.
Hata hivyo, kamanda Lyanga, alisema maeneo ya Mkuranga hadi Utete na Rufiji yanaandamwa na uhalifu mbalimbali hivyo jeshi hilo limejipanga kupambana na wahalifu.
Aliwataka wananchi kuacha kuwakumbatia wahalifu wanaowafahamu kisa jirani ama ndugu bali washirikiane na jeshi hilo kwa kuwafichua ili kuwachukulia hatua za kisheria.
Kamanda Lyanga alisema hawatakuwa na huruma kwa wahalifu wanaotumia silaha, kupora, unyang'anyi kwani wanakosea amani raia walio wema.
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania