CURRENT NEWS

Saturday, March 4, 2017

MKUTANO WA TANO WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR WAHITIMISHWA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tano wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar huko Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafungua tena kazi za uchimbaji  mchanga kuanzia Jumatatu ya Tarehe 6 Machi 2017 ikilazimika kuchukuwa uamuzi mgumu wa kusimamia moja kwa moja uchimbaji huo badala ya kuwaachia Wananchi.

Alisema maamuzi hayo ya Serikali yatakwenda sambamba na utolewaji wa bei elekezi ya mchanga ili kujaribu kuzuia uharibifu wa mazingira uliokwishaathiri maeneo mengi yaliyokwishachimbwa mchanga pamoja naulanguzi wa kupita kiasi kwa wauzaji wa rasilmali hiyo.

Akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tano wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar huko Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wizara ya Kilimo itaandaa  zamu za kuchimba mchanga ili kupunguza msongamano wa gari zitakazokwenda katika maeneo ya Mchanga.
Alisema zamu hizo zitawapa fursa ya siku Tatu  kwa Wiki Wananchi wa kawaida kupata rasilmali hiyo ya Mchanga na Siku Mbili kwa Wiki zitazingatiwa kwa Makampuni na Taasisi  za Serikali  zilizopata vibali vya Ujenzi wakati Jumamosi na Jumapili zitakuwa siku za mapumziko.

Balozi Seif alisema utafiti unaendelea kufanywa na Kamati ya Wataalamu kwa kushirikiana na ile ya Mawaziri inayoshughulikia suala mchanga kujua kiwango cha mchanga kiliopo kwenye eneo la Kiwanda cha Sukari Pangatupu, Kichwele na maeneo mengi ili kubaini wingi wake  na endapo utafaa kwa matumizi ya ujenzi.
Alisema Zanzibar si nchi ya kwanza kuwa na upungufu wa mchanga ambapo ipo mifano ya uhaba wa rasilmali hiyo iliyokwishajitokeza katika baadhi ya nchi duniani kama vile Malaysia, Singapore, Phillipines na Tuvalu.

Balozi Seif alieleza kwamba upo ushahidi wa wazi uliothibitisha kuzama kwa Visiwa vodogo vidogo Vitano Nchini Phillipines kufuatia wimbi kubwa la uchimbaji wa mchanga kiholela pembezoni mwa fukwe zilizokuwa zimevizunguuka Visiwa hivyo.

Alifahamisha kwamba ushibiti huo wa rasilmali ya mchanga unaweza kupelekea Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini wakavamia fukwe kuchota mchanga. Hivyo aliziomba mamlaka zote kupiga marufuku uchotaji huo ili kujiepusha na majanga na kuangamiza Visiwa hivi.

Alitahadharisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia vyombo vyake itatoa adhabu kali kwa mtu ye yote atakayekwenda kinyume dhidi ya agizo lililotolewa na Serikali kuhusu suala zima la uchimbaji wa Mchanga.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakisikiliza Hotuba ya kuahirishwa kwa Mkutano wa Tano wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani. Picha na – OMPR – ZNZ.

Akizungumzia vita dhidi ya Dawa za kulevya vilivyotangazwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alionya kwamba Zanzibar haitakua kimbilio la waendelezaji wa biashara hiyo haramu na badala yake itakuwa gereza lao.

Balozi Seif  alisema vita hivyo ni vya Nchi nzima ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar. Hivyo wale wanaofikiria kwamba vita hivyo ni kwa Tanzania Bara pekee wanaelezwa bayana kuwa wamepotea njia.

Alisema Takwimu kutoka Tume ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya zinaonyesha kwamba mwaka 2016 jumla ya kesi 37 ziliripotiwa kwenye Mahakama za Unguja na Pemba na ni Mtu Mmoja tu ndie aliyetiwa hatiani.

Akigusia vita dhidi ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema bado lipo ongezeko kubwa la vitendo hivyo vinavyoshinda kutoa matunda mazuri yaliyokusudiwa.

Alisema takwimu za vitendo hivyo viovu zilizoripotiwa kuanzia mwezi Julai hadi Septemba Mwaka 2016 zinazonyesha jumla ya matukio 218 yamewasilishwa katika vyombo vinavyohusika Unguja na Pemba.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba hali hiyo bado inatisha na kutoa ujumbe kuwa bado Jamii inahitaji kushirikiana kwa karibu kujaribu kutokomeza vitendo vya udhalilishaji vya Kijinsia hapa Nchini.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar  limeahirishwa hadi Jumatano ya Tareje 10 Mwezi Mei mwaka 2017.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania