CURRENT NEWS

Thursday, March 23, 2017

PROF. MUHONGO ATANGAZA TAKWIMU MPYA ZA UMEME

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akitaja takwimu mpya za umeme nchini wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mikoa ya Songwe na Mbeya. Uzinduzi ulifanyika katika kijiji cha Ilinga, wilayani Rungwe. Kulia ni Titus Mwisomba, Meneja Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla (kulia) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mikoa ya Songwe na Mbeya. Uzinduzi ulifanyika katika kijiji cha Ilinga, wilayani Rungwe. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la Bluu), Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos wa Makalla (kushoto kwa Waziri) na watendaji kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA),  Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) na viongozi wa kijiji cha Ilinga wakifurahia uzinduzi  wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mikoa ya Songwe na Mbeya.

Na Teresia Mhagama, Mbeya
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametangaza takwimu mpya za kiwango cha utumiaji wa umeme nchini ambazo zinaonesha kuongezeka kwa fursa za matumizi ya umeme kwa wananchi.
Takwimu hizo amezitangaza wilayani Rungwe mkoani Mbeya, tarehe 20 Machi, 2017 wakati akizindua Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mikoa ya Mbeya na Songwe.
“Takwimu hizi zimetayarishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema kuwa hadi kufikia Desemba 2016, fursa ya kutumia umeme nchini (overall National access level) imeongezeka hadi kufikia asilimia 67.5 kutoka asilimia 10 ya mwaka 2007.
Aliongeza kuwa fursa ya kutumia umeme vijijini imeongezeka na kufikia asilimia 49.5 kutoka asilimia 2 ya mwaka 2007 na kwa mijini fursa ya kutumia umeme imeongezeka hadi kufikia asilimia 97.3.
“Tunaposema fursa katika tawimu hizi, tuna maana kuwa umeme umefika sehemu fulani na wakati wowote ukihitaji kuwekewa unaupata, hicho ni kipimo cha kwanza kinachotumika duniani wakati wa kuandaa takwimu za umeme na kipimo cha pili kinachotumika ni cha idadi ya watu waliofungiwa  umeme,” alisema ProfesaMuhongo.
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, alisema kuwa katika kila mwaka wa Fedha, kila mkoa hupewa vijiji vya kuunganishwa na huduma ya umeme huku dhamira ikiwa ni kusambaza umeme  kwenye vijiji vyote Tanzania ambavyo ni zaidi ya 12,000.
Alisema kuwa katika miradi hiyo ya umeme vijijini, Serikali imenunua vifaa mbalimbali kama nguzo, nyaya na transfoma hivyo wananchi hawatalipia vifaa hivyo wakati wa utekelezaji wa mradi bali wanachopaswa kulipia ni shilingi 27,000 tu ya kuunganishiwa umeme.
Vilevile, alisema kuwa bajeti iliyotengwa kwa ajili ya usambazaji umeme vijijini nchini ni zaidi ya shilingi Trilioni moja ambazo ni fedha za ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alipongeza juhudi za usambazaji umeme vijijini na kueleza kuwa vijiji 247 vya mkoa huo tayari vimeshapata umeme na katika REA III,  vijiji   238  vitapata umeme na kubakiwa na vijiji 8 tu.
Makalla, alitoa ombi kuwa vijiji hivyo 8 vitakavyosalia,  viwekwe katika mradi huo wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu ili vijiji vyote viwe na umeme kama ilivyo kwa makao makuu zote za wilaya katika mkoa huo ambazo zinapata huduma ya umeme.
Aidha alitoa ombi kwa Wizara na TANESCO kumaliza kero ya kukatika mara kwa mara kwa umeme mkoani humo kunakotokana na matengenezo ya miundombinu ya umeme ili Mbeya iwe na nishati ya uhakika itakayokidhi mahitaji ya majumbani na viwanda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-hanga alisema kuwa Wakala huo umeendelea kutekeza kazi ya usambazaji umeme vijijini katika mkoa wa Mbeya na Songwe ambapo mpaka sasa katika  vijiji 847,  tayari vijiji 451 vina umeme ambayo ni sawa na asilimia 53.
Alisema kuwa REA III itapeleka umeme katika vijiji 304 vya mikoa hiyo ambapo hadi kufikia machi, 2019 jumla ya vijiji 755 katika mikoa hiyo vitakuwa na umeme ambayo ni sawa na asilimia 89 ya vijiji vyote. Aliongeza kuwa vijiji 92 vilivyobaki vitaanza kusambaziwa umeme kuanzia mwaka 2019.
Mkandarasi atakayehusika na usambazaji wa umeme katika mikoa hiyo  ni kampuni ya STEG International ya Tunisia.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania