CURRENT NEWS

Sunday, March 26, 2017

PROFESA MUHONGO AZINDUA MRADI WA REA AWAMU YA TATU SINGIDA

             
Waziri wa Nishati na Madini Prof.Sospeter Muhongo  akikata  utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa utekelezaji wa  mradi wa REA awamu ya tatu katika mkoa Singida.


 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akisalimia wananchi walioshiriki uzinduzi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu.


 Waziri wa nishati na Madini prof. Sospeter Muhongo akiwakabidhi viongozi wa mkoa wa Singida mkandarasi atakayejenga mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu.

Mkuu wa wilaya ya Manyoni Godfrey Mwambe  akibonyeza kitufe kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa singida  kuashiria uzinduzi wa mradi  wa REA awamu ya tatu kwa mkoa wa Singida.

jiwe la msingi ikiwa ni uzinduzi wa mradi wa REA awamu ya tatu katika mkoa wa Singida.

                .......................................................................................................................................................

MRADI wa usambazaji umeme vijiji(REA)awamu ya tatu unatarajia kukamilisha kupeleka umeme katika vijiji 267 vilivyokuwa havina umeme katika mkoa wa Singida ifikapo mwaka 2021 kwa gharama ya shilingi bilioni 47.36.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo katika kijiji cha Mkwese kilichopo wilaya ya Manyoni mkoani Singida,waziri wa Nishati na Madini profesa Sospeter Muhongo amesema mradi huo utatekelezwa kwa hatua mbili ambapo hatua ya kwanza itahusisha vijiji 185 ambayo itatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili mpaka mwaka 2019.

 “Hatua hiyo ya kwanza utekelezaji wake umeanza mwezi  februari mwaka huu kupitia mkandarasi m/s Nakuroi Investment co ltd na awamu ya pili itaanza kutekelezwa baada ya sehemu ya kwanza kukamilika mwaka 2019 ambapo vijiji 82 vitapatiwa umeme hadi mwaka 2021,”alisema profesa Muhongo.

Aliwataka maafisa wa shirika la umeme nchini(TANESCO)kutangaza tarehe watakayofika kugawa fomu na kujiandikisha pamoja na vituo vitakavyotumika kufanya malipo ili kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata kuunganishiwa umeme kwenye ofisi za TANESCO ambazo zipo mbali na maeneo yao.

“Ujenzi wa miundombinu ni wa gharama kubwa serikali inahimiza wananchi kutumia fursa hiyo ya kuwepo kwa umeme kuboresha maisha yenu kwa kuutumia kwenye miradi ya uzalishaji mali pamoja na huduma mbalimbali za kijamii ili uwekezaji huu wa serikali ulete manufaa yaliyokusudiwa.,”alisisitiza profesa Muhongo.

Alitoa ombi kwa serikali ya vijiji kutoa ushirikiano wa kuwapatia chumba au ofisi ya kutolea huduma kwa siku watakazopanga kutoa huduma kwa kijiji husika huku akisisitiza kuwa gharama ya malipo kuunganishiwa umeme kwa njia moja ni shilingi 27,000 ambazo zitalipwa Tanesco peke yake.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa REA mhandisi Gissima Nyamo-Hanga akizungumza katika uzinduzi huo alisema  mkoa huo una jumla ya vijiji 463 ambapo kwa sasa vilivyo na umeme ni vijiji 196 sawa na asilimia 42.

“Katika REA awamu ya tatu kama ilivyokuwa katika awamu ya pili wananchi watakaounganishiwa umeme wanatakiwa kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili mkandarasi atakapofika wawe tayari kulipia na kuunganishiwa huduma hiyo,”alisema mhandisi Nyamo-Hanga.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na balozi wa Sweden na Norway ambao nchi zao zimekuwa zikisaidia kufadhili miradi ya umeme toka Uhuru ambapo walisema wanamuunga mkono  Rais John Magufuli kwa kuwa ana dhamira ya dhati ya  kuiletea Tanzania maendeleo kupitia nchi ya viwanda na kuahidi kuendelea  kusaidia miradi hiyo ili kuwarahishia wananchi huduma mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa maji,viwanda vidogo vya kusindika mazao na  kuongeza thamani ili kufikia nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.


Mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu unalenga kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji 7,873 katika mikoa yote Tanzania bara ambayo ina vijiji 12,268 ambapo hadi juni vijiji vilivyofikiwa vilikuwa 4,375 sawa na asilimia 36.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania