CURRENT NEWS

Tuesday, March 21, 2017

RAIS MAGUFULI AMEWATAKA WATANZANIA KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA ZA JUU.


Na Daudi Manongi-MAELEZO
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuulinda mradi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara za Morogoro,Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam utakaogharimu shilingi bilioni 188 na kukamilika mwaka 2019.
 
Rais Magufuli ameyasema hayo wakati akitoa hotuba kabla ya kuweka jiwe la msingi la barabara za juu eneo la Ubungo.
 
“Tutasimamia pesa izi kikamilifu ili tujenge barabara izi za juu vyema,nawataka Watanzania kusimamia mradi huu ili ukamilike haraka na hivyo Wizara,Mkandarasi na Msimamizi wa mradi ili ulete ukamilike na kuleta tija kwa wananchi hawa”,Aliongeza Rais Magufuli.
 
Amesema katika ujenzi wa mradi huo bilioni 1.9 inatoka Serikalini na bilioni 186 inatoka Benki ya Dunia na ivyo ni muhimu kuulinda kwani ni pesa za Watanzania walipa kodi.
 
Aidha amesisitiza kuwa nchi ya yetu imepata mkopo huu  kwa sababu tunaaminika katika kukopesheka na tunarudisha kwa wakati,amemuomba rais wa benki ya Dunia  kuendelea kuikopesha Tanzania katika miradi mingine.
 
Rais Magufuli ameeleza kuwa mkopo huu kutoka benki ya Dunia una riba ya asilimia 0.5 na unalipwa ndani ya miaka 40 ivyo ni vyema kuendelea kushirikiana na Benki ya Dunia.
 
Pamoja na hayo amewataka Watanzania kuendelea kulipa kodi itakayowezesha ili Serikali iendelee kutekeleza miradi mingine na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu kutatoa sura ya pekee ya jiji la Dar es Salaam na kupunguza msogamano wa magari kwa kiasi kikubwa sana.
 
Kwa Upande wake Rais wa Benki ya Dunia Dkt.Jim Yong Kim ametoa shukurani kwa Serikali ya Tanzania na kusema kuwa ameshawishika kuja nchini baada ya kusikia vongozi wengi wa Dunia wakisifia jitihada za Rais Magufuli za kuunda upya Serikali yake ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi na kuwekeza katika kujenga miundombinu na elimu.
 
“Tanzania inaelekea kuwa Taifa la watu wa kipato cha kati miaka nane ijayo na kila mtu kuwa na bima ya afya,elimu bora na muono mzuri wa mbeleni,na njia pekee ya kufika huko ni kujitegemea na kutumia rasilimali za nyumbani katika mkakati bora kabisa na hivyo kupunguza kabisa misaada ya nje ambayo imeshuka hapa nchini kwenu,”Aliongeza Dkt.Jim Yong Kim
 
Aidha amesema kuwa tangu kufunguliwa kwa Mabasi ya Mwendo kasi imepunguza msongamano kwa dakika 90 kwa siku na hivyo ufunguzi wa biashara mpya pia umeenda sambamba.
 
Amesisitiza kuwa Benki ya Dunia itaendelea kusimama pamoja na Tanzania katika maendeleo na kufanya kazi pamoja.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania