CURRENT NEWS

Wednesday, March 1, 2017

RC NCHIMBI AITAKA KAMATI YA SAIDIA MICHEZO SINGIDA KUJIPANGA KWA AJILI YA LIGI KUU.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Saidia Michezo  Miraji Mtaturu akimkabidhi Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Rehema Nchimbi taarifa ya timu ya  Singida united  kupanda ligi kuu na mipango ya maandalizi ya kushiriki ligi kuu inayotarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti mwaka huu.
  Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Saidia Michezo ya mkoani Singida akimsikiliza mkuu wa mkoa huo Dk.Rehema Nchimbi baada ya kumkabidhi taarifa ya timu ya  Singida united  kupanda ligi kuu na mipango ya maandalizi ya kushiriki ligi kuu inayotarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti mwaka huu.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Rehema Nchimbi akiwa ofisini kwake na baadhi ya wajumbe wa kamati ya Saidia Michezo ambao ni mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu na Mbunge wa Singida Mjini Mussa Sima baada ya kumkabidhi taarifa ya timu ya  Singida united  kupanda ligi kuu na mipango ya maandalizi ya kushiriki ligi kuu inayotarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti mwaka huu.
            .............................................................
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.Rehema Nchimbi ameitaka kamati ya Saidia Michezo mkoani humo kujipanga vizuri kuhakikisha timu ya Singida United inafanya vizuri katika mashindano ya  ligi kuu Tanzania Bara yanayotarajiwa kuanza mapema  mwezi Agosti mwaka huu.

Timu hiyo ilipata nafasi ya kuingia katika mashindano ya ligi kuu baada ya kuipa kipigo cha magoli 2-1  timu ya Alliance ya Mwanza.

Akizungumza ofisini kwake wakati akipokea taarifa ya kupanda daraja timu hiyo kucheza ligi kuu na mipango ya maandalizi ya kushiriki ligi hiyo, Dk.Nchimbi alisema kamati hiyo ina kila sababu ya kuweka maandalizi vizuri ili lengo la mkoa la kuibuka na ushindi liweze kufanikiwa.

“Jukumu hili lisiachiwe kwa kamati peke yake bali pia wadau wa soka wadau wa timu yetu tuendelee kuunga mkono timu yeti ili iwe tayari kupambana katika mechi zijazo,”alisema Nchimbi.

Aliipongeza kamati ya Saidia Michezo,wadau wa soka,viongozi wa timu na wachezaji kwa juhudi walizozionyesha na kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imezaa matunda ya ushindi kwa timu kuweza kupanda daraja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo Miraji Mtaturu ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi akikabidhi taarifa kwa Mkuu huyo mkoa,  alisema ushindi uliopatikana umekidhi kiu ya muda mrefu ya wana Singida waliyokuwa nayo kwa takribani miaka 17 sasa na kuahidi kwa niaba ya kamati kuendeleza mazuri yote yaliyopelekea kupatikana kwa ushindi.

“Kamati yetu ina wajumbe takribani 12 na ushindi huu umepatikana kutokana na mshikamano uliopo miongoni mwetu ,dhamira ya dhati miongoni mwa wajumbe,uongozi wa timu,wachezaji,walimu wa timu,serikali,viongozi wa Chama Cha Soka  Sirefa,na wapenzi wa soka kwa ujumla jambo ambalo kama kamati tunaahidi mbele yako tutayaenzi na kuyaendeleza haya,”alisema Mtaturu.

Alitaja moja ya mipango waliyonayo kuwa ni kuurekebisha uwanja wa Namfua ili uweze kukidhi vigezo vilivyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini(TFF).
 
Hivi karibuni timu hiyo ilifanikiwa kupanda daraja hadi ligi kuu baada ya kufanya vizuri katika ligi daraja la kwanza ambapo ilikuwa katika kundi C pamoja na timu ya Alliance academia, Polisi Mara, Polisi Dodoma, Rhino Rangers, Panone ya Moshi na Mgambo JKT.

Singida United kwa sasa ina miaka 45 ambapo kama ni mtoto tayari ameshakuwa na ana mji wake,mwasisi wa timu hii ni marehemu Elisamwel Elisamwel aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Maji kwa wakati huo Singida Mjini ambapo kutokana na sababu mbalimbali ilishuka daraja msimu wa 2001/2002 mpaka 2013 ilipofufuka tena na kuanza harakati ya kurejesha heshima ya soka mkoani Singida.


Kupanda daraja kwa timu hiyo sio tu kutainua mkoa kisoka bali pia kutaongeza uchumi wa wananchi na mkoa kwa ujumla.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania