CURRENT NEWS

Monday, March 27, 2017

RC NDIKILO AGEUKA MBOGO KWA VYAMA USHIRIKA VYA MSINGI VYA KOROSHO(AMCOS)

Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo, akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi wilaya ya Mkuranga. (picha na Mwamvua Mwinyi)


Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo,ametoa wiki mbili kwa vyama vya ushirika vya msingi vya korosho,vya Rifiji, Kibiti na Mkuranga,kwenda kujieleza kwa wakuu wa wilaya zao kuhusu upotevu wa mamilioni ya fedha.

Aidha amewaasa kuacha tabia ya wizi kwa wanunuzi na kuhujumu zao hilo la biashara.
Mhandisi Ndikilo pia amekemea tabia ya wanunuzi wanaochelewa kulipia korosho na kuziacha kwenye maghala kwa muda mrefu.
Akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi wilayani Rufiji, Kibiti na Mkuranga, alitaka vitendo hivyo visijirudie katika msimu ujao.
Mkuu huyo wa mkoa, alieleza kwamba, Bungu B Amcos wamemuuzia mnunuzi tani 320 ambapo alikuta 298 huku  tani 22 zikiwa hazipo zenye gharama ya sh. Mil 72.9.
"Bungu Amcos mnunuzi alikuta tani 11 hazipo zenye thamani ya mil. 33.
"Bungu Mahege mil. 12 zimetiwa mfukoni, Mjawa Amcos tani 4 zimepigwa zilizogharimu mil. 11"alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo, alielezea kuwa, hawezi kukubali kuona vyama vya ushirika vinashiriki kuupa mkoa fedheha.
Alifafanua kuwa, vyama vilivyojihusisha kutapeli wanunuzi vitoe sababu za msingi kwa wakuu wa wilaya kueleza ubadhilifu huo na wakibainika kufanya wizi vyombo vya sheria vifanyekazi yake.
Akizungumzia mfumo wa stakabadhi ghalani aliomba utumike vizuri kwani bila kufanya hivyo utateteleka.
Mhandisi Ndikilo alisema ni lazima haki itendeke ili wakulima wanufaike badala ya kuwabana kwa kuwapa masharti magumu hali itakayosababisha kuondoa imani na mfumo huo ambao ndio unawanufaisha kwa sasa.
Hata hivyo alisema wanunuzi wa korosho wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kulipa wakulima katika muda stahiki .
“Safari hiii atakaebainika kufanya ujanja ujanja tutamfunga, na hapo ndipo mtajua kama mna RC mkali ,msile jasho la wanyonge ,"alisisitiza.
Mbali ya hilo, mhandisi Ndikilo, alihimiza kilimo cha mazao yanayohimili ukame ikiwemo muhogo, kunde ili kujiepesha na baa la njaa.
Katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji, Shangwe Twamala alisema, wataalamu kutoka bodi ya korosho ndio wana hakiki ubora wa korosho katika vyama vyote vya msingi vilivyokusanya korosho kwa kushirikiana na CORECU na kisha kuandaa muongozo kwa wanunuzi.
Alisema muongozo wa mauzo namba 1 wa mwaka 2015,kifungu namba 4.4 wa bodi ya korosho Tanzania  kinasema mnunuzi ataruhusiwa kuhakiki ubora wa korosho zilizopo kwenye ghala baada ya kufanya utaratibu wa kulipa korosho .
Twamala alieleza, baada ya malipo mnunuzi ataruhusiwa kuhakiki baada ya kufanya utaratibu huo atapewa idhini ya kwenda na mwendesha ghala ama bodi ya korosho kwa maandishi .
Kwa upande wao viongozi wa Amcos hizo, akiwemo mwenyekiti wa Kibiti Amcos Saidi Lipenda, alisema matajiri, wanunuzi waangaliwe wasitake kuvuruga mkoa.
Nae kiongozi wa Bungu B Amcos, Sada Omary,alisema korosho zikiwa mbichi kwenye maghala zikija kukauka tani zinapungua.
Alieleza wanunuzi waache kung'ang'aniza kupima.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania