CURRENT NEWS

Friday, March 3, 2017

SHIRIKA LA HAPA LA UJERUMANI KUWAJENGEA ZAHANATI WANANCHI WA KIJIJI CHA NG’ONGOSORO WILAYANI IKUNGI

        
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akipewa maelezo ya ujenzi wa nyumba ya waganga wa Zahanati kutoka kwa msimamizi wa Mradi huo Stanford Mkude huku Katibu Tawala wa wilaya hiyo  Winfrida Funto na kaimu mkurugenzi wa HAPA  Noel Makyao wakisikiliza, 
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akijaribu pampu ya mkono ya kuvutia maji katika eneo la zahanati huku Diwani wa kata ya Isuna  Stephano Misai, katibu tawala wa wilaya Winfrida Funto na kaimu mkurugenzi wa HAPA Noel Makyao wakishuhudia.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akipata maelezo kutoka kwa  mwenyekiti wa kitongoji cha mbugani Sita Dui juu kwa nini jamii haishiriki kujitolea kutoa nguvu kazi kwa mujibu wa mkataba waliowekeana na mfadhili na halmashauri. 
Wananchi wa tarafa ya Ikungi waliohudhuria mkutano wa hadhara wakimsikikiza Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu (hayupo pichani) wakati akihutubia ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kila alhamisi kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo.

                .......................................................................................................................

WANANCHI wa Kijiji cha Ng`ongosoro wilaya ya Ikungi wapo mbioni kuondokana adha  ya kutembea umbali mrefu wa kilomita 32 kufuata huduma za afya baada ya shirika lisilo la kiserikali la HAPA la nchini Ujerumani linalojishughulisha na uboreshaji wa afya ya jamii katika Nyanja za elimu,afya,maji na usafi wa mazingira kufadhili ujenzi wa zahanati ili kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Ukamilikaji wa Zahanati hiyo ni hatua moja wapo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2015-2020 inayoeleza utekelezaji wa Mpango wa maendeleo wa Afya ya msingi(MMAM) wenye lengo la kuimarisha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuhakikisha kunakuwa na Zahanti kila kijiji,kituo cha afya kila kata na hospitali katika kila wilaya.

Akitoa taarifa ya miradi mbele ya mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu aliyekuwa katika ziara Tarafa ya Ikungi mkurugenzi wa HAPA Jochen Muller alisema kwa sasa Zahanati imekamilika na ujenzi wa nyumba mbili za waganga wa Zahanati zinaendelea ambapo pia wanajenga  madarasa mawili,nyumba ya walimu na kuchimba visima vitano katika kijiji hicho kwa gharama ya zaidi ya milioni 191.

 “Katika kutekeleza miradi hii tulianza na ujenzi wa madarasa mawili ambayo yamekamilika,tumechimba visima vitano kwenye vitongoji vya kijiji hiki na sasa tupo kwenye zahanati lakini lengo letu ni kuhakikisha hadi machi 31 tunakabidhi mradi tayari kwa kutoa huduma,”alisema Josen.

Alieleza changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni jamii kutoshiriki kuchangia nguvu kazi katika vifaa vinavyopatikana kama mawe,mchanga na kumwagilia maji matofali kama walivyokubaliana awali hali inayosababisha mkandarasi kukosa vitu hivyo kwa wakati na hivyo kupelekea mradi kushindwa kukamilika kwa muda uliopangwa.

Akizungumza baada ya kupokea changamoto hizo mkuu wa wilaya hiyo Mtaturu aliuelekeza uongozi wa kijiji kupanga ratiba ya kila jumanne na alhamisi kwa wananchi kushiriki kazi katika   ujenzi wa miradi ya maendeleo inayoendelea ili iweze kukamilika kwa wakati.

Aidha alimuagiza mkugurugenzi kumpeleka muuguzi ifikapo machi 7 ili aanze kutoa huduma za awali katika zahanati hiyo na kukitaka kijiji kutafuta hifadhi ya nyumba ya muda kwa ajili ya kuishi muuguzi huyo na kuwataka wahusika wote kutimiza wajibu wao ili aprili 4  azindue zahanati rasmi na kutoa huduma kwa wananchi.

“Nawashukuru wafadhili kwa kusaidia ujenzi wa miradi hii ambayo ina manufaa makubwa kwa wananchi,naomba niwaahidi tu kuwa yale yanayohusu serikali tutayatekeleza na ninaomba wananchi mthamini mchango wa wafadhili hawa na mtimize majukumu yenu kama mlivyokubaliana,”aliongeza Mtaturu.

Mikakati iliyojiwekea kama wilaya ni kuhakikisha wanapunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kuhakikisha wanajenga Zahanati kila kijiji kama Ilani ya CCM inavyotaka na kuweka clinic inayotembea katika maeneo ambayo hayana Zahanati lakini imezindua daftari la ufuatiliaji wa wajawazito kila kitongoji tangu agosti mwaka jana.


Ziara hiyo ya mkuu huyo wa wilaya ni muendelezo wa utaratibu wake aliojiwekea wa kila siku ya alhamisi kuhamishia ofisi yake katika tarafa lengo likiwa ni kutembelea miradi inayoendelea kutekelezwa na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania