CURRENT NEWS

Tuesday, March 28, 2017

WADAU WAMIMINIKA KUMUUNGA MKONO JUMAA KUCHANGIA UJENZI WA UZIO KITUO CHA AFYA MLANDIZI

Mbunge wa jimbo la  Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akionyesha mifuko ya saruji 500 aliyochangiwa na wadau mbalimbali ili kusaidia katika ujenzi wa uzio wa kituo cha afya Mlandizi,ambao umezinduliwa rasmi .
Mbunge wa jimbo la  Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akishiriki nguvu kazi na baadhi ya wananchi katika uzinduzi rasmi wa ujenzi wa uzio wa kituo cha afya Mlandizi .(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
WADAU na viongozi mbalimbali jimbo la Kibaha Vijijini,wamejitokeza kumuunga mkono mbunge wa jimbo hilo, Hamoud Jumaa kufanikisha ujenzi wa uzio wa kituo cha afya Mlandizi.
Ujenzi huo unatarajiwa kugharimu mil. 200 na ukikamilika utaondoa kero hiyo iliyodumu miaka mingi .
Jumaa aliyasema hayo baada ya uzinduzi rasmi wa ujenzi huo ambapo hivi karibuni alianza kwa kuweka alama ya msingi.
Alieleza kwamba, wameshakubaliana na wananchi na wenyeviti wa vitongozi 26 kuwa kila kitongoji kitachangia sh.240,000 .
"Madiwani kila mmoja atachangia 240,000 hivyo wanatarajia kukusanya zaidi ya sh. mil.4, mfuko wa jimbo sh. mil. 4 kununulia tofali zitakazoanzia ujenzi"alisema .
Hata hivyo,tayari wadau wamemkabidhi mifuko 500 ya saruji iliyogharimu sh. mil. 6, kokoto tani 7 kwa sh. mil. 9.1, mchanga mil. 2.4 tofali sh. mil 8.4, nondo tani moja sh. mil. 3.6.
Jumaa alisema ,kwa msingi kero ya ukosefu wa uzio ni kubwa inayosababisha usumbufu kwa wagonjwa kutokana na watu,pikipiki kupita na kupiga kelele.
Alieleza kuwa ujenzi huo utafanyika kwa awamu nne ambapo awamu ya kwanza unatarajia kutumia zaidi ya sh. mil. 40.
Baada ya uchimbaji wa msingi itafuata kumimina zege kisha kuanza ujenzi wa tofali na awamu hiyo itachukua wiki mbili.
Jumaa alisema hadi sasa ni juhudi za mbunge na wafadhili ambazo wanategemea kuanza ukuta wa mbele, kuchimba msingi na kumwaga zege .
"Tumezindua rasmi ujenzi ,lengo ni kutekeleza moja ya vigezo vya kituo chetu kupanda hadhi ya hospitali ya wilaya"
Alitaja vigezo vinavyotakiwa kuwa ni pamoja na kuwepo kwa chumba cha upasuaji na kuhifadhia maiti ,kuongeza watumishi wa afya, madaktari na kigezo kikubwa ni ujenzi wa ukuta.
Jumaa alisema, kwa sasa amejipanga kwenda sambamba na kauli mbiu yake ya "Sisi kwanza serikali baadae ".
Anawaomba wadau wa afya na serikali kuendelea kumuunga mkono ili tatizo hilo libakie historia.
Mbunge huyo alimshukuru makamu wa Rais mama Samia Suluhu kwa kuahidi kushirikiana nae kujenga uzio huo.
Diwani wa kata ya Mlandizi Ephrasia Kadala alimpongeza Jumaa kwa kuanzisha suala hilo na kusema kwa muda mrefu kituo hicho kilikuwa kikipata usumbufu.
Makamu Mwenyekiti Godfrey Mwafulilwa alisema walipokea wazo la ujenzi kutoka kwa mbunge huyo kwenye kikao ambapo alishauri kwenye mpango wa mwaka 2016/2017 halmashauri iangalie namna ya kuchangia.
Tatu Jalala Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlandizi alisema wamekubaliana kila  mwenyekiti wa Mji huo atachangia sh.240,000 kwa ajili ya ujenzi huo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania