CURRENT NEWS

Thursday, March 30, 2017

WANACCM PWANI WATAKIWA KUCHAGUA VIONGOZI WENYE UWEZO ILI KUJENGA DARAJA LA USHINDI 2020


 Katibu wa CCM mkoa wa Pwani, Hassan Mtenga akizungumza na wanaccm Rufiji. 
Katibu msaidizi mkuu wa CCM Mkoa wa Pwani, Abihudi Shilla akizungumza.(picha zote na Mwamvua Mwinyi)


Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
CHAMA cha Mapinduzi (CCM),mkoani Pwani, kimewataka wanachama kuchagua viongozi wenye uwezo katika chaguzi mbalimbali za chama zijazo ili kukijenga daraja la kushika dola 2020 .
Aidha kimekemea tabia ya baadhi ya watendaji kuweka safu zao hali inayosababisha wanachama wengine kukosa nafasi.
Mbali ya hayo,vijana wamehimizwa kujitokeza kuchukua fomu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Akizungumza katika ziara yake ya mikutano ya ndani, wilayani Rufiji, katibu wa CCM mkoani hapo, Hassan Mtenga, alisema wapo baadhi ya watendaji wanaoweka safu zao.
Aliwataka makatibu hao wa CCM kuwapa fomu wale wote wenye nia ya kugombea pasipo kuwabania .
"Kumekuwa na kijitabia kwa baadhi ya makatibu kuwanyima fomu wanachama ambao sio safu yao jambo ambalo linashusha sifa ya chama "alisema Mtenga.
Mtenga alieleza kwamba, ni wakati wa kutoa fursa ya ushindani kwa makundi yote yanayojitokeza .
Akizungumzia lengo la ziara hiyo, alisema kwamba, inalenga kutoa elimu kwa wanachama wenye nia ya kugombea na kuwahamasisha.
Pia kuwaambia marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2012 na marekebisho ya kanuni za uchaguzi ili ziendane na marekebisho ya katiba hiyo.
Nae katibu msaidizi mkuu wa CCM wa mkoa huo, Abihudi Shilla, aliwataka wanachama wa CCM wajitokeze kwa wingi kugombea uongozi katika nafasi hususan za mashina ,matawi na ngazi zote za uongozi.
Aliwaasa viongozi kutoa fomu kwa uwazi ili kila mwenye sifa aweze kuchukua na kujaza fomu hizo.
Wakiwa Rufiji walizungumza na wanachama na viongozi katika kata ya Kipugila, Ngolongo, Mkongo, Mbwara, Muhoro, Chumbi na Ikwiriri.
Ziara hiyo inaendelea wilaya ya Kibiti na Mkuranga .
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania