CURRENT NEWS

Monday, March 13, 2017

WATU ZAIDI YA 20 KATI YA 2,000,HUKO VIGWAZA WAUGUA MTOTO WA JICHO

Mkazi wa Vigwaza Sale Juma akipimwa jicho katika kambi ya huduma ya macho iliyofanywa na Lions club dar es salaam -Panorama huko shule ya msingi Vigwaza.
 Diwani wa kata ya Vigwaza, Mohsin Bharwani akizungumza na baadhi ya wakazi waliojitokeza kwenye kambi ya macho iliyofanywa na Lions club dar es salaam -Panorama huko Vigwaza. (picha na Mwamvua Mwinyi)
 Baadhi ya wakazi wa kata ya Vigwaza,waliojitokeza kkwenye kambi ya huduma ya macho iliyofanywa na Lions club dar es salaam -Panorama, wakisikiliza jambo katika kambi hiyo.

Na Mwamvua Mwinyi, Vigwaza
WAKAZI zaidi ya 20 kata ya Vigwaza, wilayani Bagamoyo,Pwani, wanatakiwa kufanyiwa upasuaji ili kutibu ugonjwa  wa mtoto wa jicho.
Aidha taasisi hiyo imetoa madaftari na vitabu vilivyogharimu sh.mil sita katika shule mbalimbali kwenye kata hiyo.
Akitoa taarifa katika kambi ya macho iliyofanyika shule ya msingi Vigwaza ,mratibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya lions dar es salaam -PANORAMA, Prash Bhatti, alisema huduma ya macho waliyoitoa imegharimu mil. 30.
Alisema mbali ya kutoa huduma za macho ,pia waliwahudumia wagonjwa wa kisukari, presha na kusaidia huduma za kijamii.
Hata hivyo Bhatti alisema kambi hiyo ilikuwa ni ya siku mbili ambapo watu 2,000 walijitokeza kupima macho na kupata huduma ya miwani bure .
"Shida kubwa ni ugonjwa wa mtoto wa jicho ambao kitaalamu tunaita cataract ugonjwa huu ndio unaoongoza kwa kuharibu jicho, dawa  yake  ni upasuaji"alisema.
Bhatti alielezea,watu hao waliogundulika na mtoto wa jicho watafanyiwa upasuaji na  gharama zote zitatolewa na  lions club.
Alisema tatizo hilo la  mtoto wa jicho lisipopata matibabu mapema husababisha upofu na kusababisha mtu kuishi katika hali y'all umaskini.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,alitoa wito kwa jamii kupima macho mara kwa mara ili tatizo libainike mapema na kutibiwa.
Aliiasa jamiii kufanya matibabu ya mtoto wa jicho  hospitali badala ya kukaa majumbani bila kujitibia.
Mhandisi Ndikilo, alisema tiba ya ugonjwa huo  ni upasuaji na kuwa ulaji mzuri wa chakula na matunda hukinga macho dhidi ya magonjwa mbalimbali.
"Nampongeza diwani wa kata hii Mohsin Bharwani kwa kuona umuhimu wa kuwatumikia wananchi wake ikiwemo masuala ya kiafya"alisema mhandisi Ndikilo.
Diwani wa kata ya Vigwaza, Mohsin Bharwani aliishukuru taasisi hiyo kwa kujitolea kutoa huduma mbalimbali za afya na vitabu mashuleni.
Alifafanua kwamba watu wengi huwa hawapendi kuchunguza afya zao hivyo lions club imekuwa mkombozi kwao.
Bharwani, alishukuru pia kupokea msaada wa vitabu na madaftari kwa wanafunzi wa shule zilizopo Vigwaza.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania