CURRENT NEWS

Monday, April 10, 2017

MBUNGE RIDHIWANI AAHIDI KUSIMAMIA TATIZO LA BARABARA


MBUNGE wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,akiangalia barabara kutoka Vigwaza-Mwavi iliyoharibika vibaya eneo la Buyuni hali inayosababisha magari kushindwa kupita.

 Mkazi wa Mwavi ,Zainab Zuberi akivushwa  kwenye maji yaliyokata barabara eneo la Buyuni,kwa kubembwa shingoni .

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,akizungumzia kero ya kuharibika kwa baadhi ya  miundombinu ya barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha,ambapo mvua iliyonyesha april 7 na 8 imesababisha kuharibu barabara ya Vigwaza-Buyuni-Mwavi na ya Milo-Kitonga-Ruvu.

Baadhi ya wakazi wanaotumia barabara ya Vigwaza-Buyuni-Mwavi wakipita kwa shida kutoka na barabara hiyo kuharibika vibaya kutokana na mvua.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la Chalinze,Ridhiwani Kikwete aahidi kusimamia tatizo la barabara ya Vigwaza-Mwavi eneo la Buyuni,ambayo imekata mawasiliano kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Alisema ,hali iliyopo hairidhishi na kuwapa wakati mgumu wakazi wa maeneo hayo.
Ridhiwani ameeleza ataifikisha changamoto hiyo,bungeni na halmashauri ya wilaya ya Chalinze ili lifanyiwe kazi.
Katika hatua nyingine ameunga mkono juhudi za ujenzi wa darasa lililobomoka kutokana na mvua iliyonyesha april 7 ambapo amechangia kiasi cha sh.100,000,mabati 50,mifuko ya saruji 50 na nondo 20.
Ridhiwani,aliyasema hayo,mara baada ya kutembelea barabara hiyo kujionea hali halisi iliyopo.
Alieleza kuna kila sababu ya mkandarasi kufanya kazi kulingana na uhalisia wa eneo husika hali inayosababisha wananchi kupata tabu na barabara kuharibika kila wakati.
Kwa upande wa vijana wanaosaidia kuvusha watu katika eneo hilo,akiwemo Majid Juma,alisema mvuakubwa iliyoambata na upepo mkali,imekata mawasiliano ya barabara hiyo na kusababisha wakazi kutoka kata ya Vigwaza na Mwavi jimbo la Chalinze,kupata shida.
"Hali hii inasababisha wakazi hao,kuvushwa kwa kupata msaada wa kubebwa mgongoni na shingoni kwa gharama ya sh.3,000 na 2,000 na pikipiki kupitishwa kwa sh.5,000 huku magari yakishindwa kupita kabisa"alisema Juma.


Juma alibainisha kwamba,tangu mvua ziharibu eneo hilo april 7 wanavusha watu kwa maelewano kulingana na uwezo wa mtu.
“Tunapata fedha kulingana na kichwa cha mtu au pikipiki,kila mtu mmoja 3,000 au 2,000 na pikipiki 5,000 “alieleza.
Baadhi ya wakazi wa Mwavi ,akiwemo Zaina Zuberi aliekuwa akienda Mwavi,alisema wapo katika hali ngumu .
“Mvua hapa bado haijanyesha,maji haya yanatokea maeneo ya Msoga huko na kufika huku daraja la Mbiki,Buyuni na kukatiza katika hii barabara,sipati picha mvua ikipiga hapa kwa mwezi huu”
“Barabara ni mbovu kama mnavyojionea,haipitiki,watu tunapata shida kufuata mahitaji ya nyumbani ,tatizo ni mkandarasi ,barabara imejengwa bila kuwekwa makaravati,kila akielekezwa kujenga kutokana na hali halisi ya barabara haiwi hivyo,”
Katika hatua nyingine kutokana na mvua hizo,zimeathiri pia barabara nyingine ya kutoka Milo-Kitonga hadi Vigwaza.

Mbali ya hayo,Ridhiwani ameunga mkono ujenzi darasa katika shule ya msingi  Kidogozero ambalo imebomoka kutokana na mvua.

Afisa mtendaji  wa Kidogozero,Lilian Mbwa,alisema kila kaya itachangia matofali mawili na kila mjumbe wa serikali ya kijiji ni tofali 10.
Hata hivyo alisema halmashauri ya kijiji itachangia jumla matofali 200 na wadau wa maendeleo matofali 300.
Mwishoni mwa wiki iliyopita,kaya zaidi ya 20 zimekosa makazi ya kuishi na nyumba zaidi ya  100ziliharibika ,kubomoka na nyingine kuezuliwa mapaa huko jimbo la Chalinze,kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania