CURRENT NEWS

Monday, April 10, 2017

DC BAGAMOYO AWAOMBA WADAU NA JAMII KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUSAIDIA WAHANGA WA MAFURIKOMkuu wa wilaya ya Bagamoyo, alhaj Majid Mwanga, akitembelea miundombinu mbalimbali hususan ya barabara iliyoharibika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. (picha na Mwamvua Mwinyi) 
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
MKUU wa wilaya ya Bagamoyo,mkoani Pwani alhaj Majid Mwanga,amesema nyumba  zaidi ya nyumba 100 zilizopo kata ya Bwilingu,eneo la Chalinze Mzee na kata ya Msoga zimeharibika ,kubomoka na nyingine kuezuliwa mapaa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kufuatia maafa hayo ,amewaomba wadau mbalimbali wa jamii kujitokeza kusaidiana na serikali kuwasaidia wahanga wa mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha  kuanzia april 7 hadi 8.
Aidha alhaj Mwanga, ametoa rai kwa jamii kuendelea kusaidiana kwa sasa wakati serikali ikiendelea kutafakari namna ya kushirikiana na wadau .
Mvua hizo zimeathiri baadhi ya maeneo ya Msoga,Chalinze Mzee,darasa moja katika shule ya msingi Kidogozero, Bwawa la umwangiliaji la Msoga ambalo limetoboka na shule ya Sekondari ya Imperial.
Akizungumza na baadhi ya wakazi waliokumbwa na maafa hayo na waandishi wa habari, mara baada ya kutembelea maeneo hayo,alhaj Mwanga , alisema kwasasa majirani,ndugu na jamaa waendelea kusaidiaana .
Alieleza kuwa hatua zitakazofuata zitakuwa ni ziada pekee lakini haina budi kusema ukweli kuwa kilichopo sasa ni jamii kusaidia yenyewe kwa yenyewe.
“Serikali inatafakari cha kufanya kutafuta wadao,ila tuende na ukweli lazima muhakikishe mnasaidiana wenyewe kwa wenyewe pasipo kuitegemea serikali pekee”
“Nashukuru hakuna maafa makubwa makubwa ya vifo na majeruhi zaidi ya kubomoka kwa nyumba  na kuharibika ambapo wahusika wamepata hasara kubwa”alieleza alhaj Mwanga. 
Baadhi ya wakazi akiwemo mzee Rashid Mwinyigoha ,alisema mvua hiyo ni kubwa na haijawahi kutokea ambayo imewapa hasara kubwa.

Alibainisha kuwa hali hairidhishi kwani nguo,fedha,chakula  na vitu vyote vimeondoka na maji hivyo hawana la kufanya.
Kwa upande wa watoto wanafunzi wanaosoma shule ya msingi Chalinze mzee wanaiomba serikali na wafadhili kuwawezesha vifaa vya shule ikiwemo madaftari,sare za shule na viatu ambavyo vimesombwa na vingine kuharibiika kwa mvua.
Diwani wa kata ya Bwilingu ,Lucas Rufunga ,alisema amepokea janga hilo kwa masikitiko makubwa na sasa wameshaanza kufanya tathmini ya awali kwa kupita nyumba hadi nyumba lakini hawajafanya tathmini ya hasara iliyopatikana .
Alisema nyumba zilizoharibika kiasi,zilizobomoka zaidi ya 100 ambapo ndani hakujabaki kitu kwa kupata hasara ya kuharibiukiwa na vitu vyao.
“Huwezi kujua nyumba hii au hiyo imegharimu kiasi gani kama risiti zinazoonyesha vifaa vya nyumba walivyonunua havipo hivyo tumefanya tathmini ya nyumba zilizobomoka na kuharibika”alisema Rufunga.
Kwa upande wake ,katibu wa mbunge  wa jimbo la Chalinze,Idd Swala,alisema Ridhiwani Kikwete anatarajia kushirikiana na diwani wa kata hiyo kusaidia wanafunzi ambao vitu vyao vya shule vimeharibika na mvua na vingine kusombwa na maji.
Ridhiwani atakachokifanya ni kuangalia namna ya kuwezesha sare kwa baadhi ya wanafunzi hao na madaftari ili kuhakikisha watoto wanaendelea na masomo baada ya sikukuu ya pasaka.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania