CURRENT NEWS

Saturday, April 15, 2017

DC MTATURU ATOA MIEZI 3 KUKAMILISHA MATUNDU YA VYOO SHULE YA MSINGI MATONGO

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akizungumza na kamati ya shule ya msingi ya Matongo na wazee na uongozi wa kijiji cha Matongo hawapo pichani  alipotembelea shule hiyo,kulia kwake ni diwani wa Kata ya Ikungi Abel Nkuwi,kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Matongo Andrea Joseph na kushoto kwake ni mwenyekiti wa kamati ya shule Joseph Benjamin na kaimu katibu tawala wa wilaya  Dandala Mzunguor.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu  akiwa kwenye  ziara katika shule ya msingi ya Matongo akikagua maendeleo ya ujenzi wa matundu ya choo pichani akikagua  shimo la choo lililofikia hatua nzuri ya ujenzi.
  
 Wajumbe wa serikali ya kijiji cha Matongo wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi hayupo pichani alipotembelea katika shule ya msingi ya Matongo.
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Matongo Joseph Benjamin akimuelezea mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu  changamoto wanazokumbana nazo shuleni hapo.

.......................................................................................................................................................

SERIKALI  ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli inafanya juhudi kubwa katika kuhakikisha watanzania wanapata maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta elimu.

Katika kutekeleza azma hiyo ineanzisha mfumo wa elimu bure uliopelekea kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi wa darasa la kwanza na hivyo kusababisha kujitokeza changamoto mbalimbali ikiwemo madawati ambayo kwa kiasi kikubwa changamoto hii imetatuliwa,vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.

Katika kuhakikisha changamoto hizo zinapungua mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu ametoa miezi mitatu kwa serikali ya kijiji cha Matongo na  kamati ya shule ya msingi ya Matongo iliyopo Kata ya Ikungi kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule hiyo.

Agizo hilo limekuja baada ya shule hiyo kukabiliwa na ukosefu wa matundu hayo hali inayosababisha wanafunzi kujisaidia vichakani na hivyo kuhatarisha afya zao na jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo shuleni hapo Mtaturu alitoa rai kwa jamii kushirikiana na uongozi wa shule katika kuhakikisha wanafanikisha ujenzi huo.

Alisema mwezi mmoja uliopita alitembelea shuleni hapo akiwa ameambatana na mbunge wa jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu na kujionea  changamoto hiyo ambapo alitoa agizo kwa kamati ya shule na serikali ya kijiji kukaa kikao cha dharura na kujadili namna ya kuanza kuandaa shimo kwa ajili ya matundu ya vyoo jambo ambalo limetekelezwa.

“Ili kufanikisha ujenzi huu katika ziara hiyo niliahidi kuwachangia shilingi milioni mbili ahadi ambayo leo naitimiza,nimewaletea matofali 1,000 yenye thamani ya shilingi  1,500,000 na  pesa taslimu 600,000 ili kusaidia kununua mifuko ya saruji muendelee na ujenzi,”alisema Mtaturu.

Alimuagiza mwalimu mkuu wa shule hiyo kutoa pesa za ukarabati zilizopo shilingi  900,000 kusaidia ujenzi huo wa  dharura na kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo Rustika Turuka kusimamia huku akiutaka uongozi wa kijiji kuacha malumbano ya kisiasa yanayozorotesha maendeleo badala yake wajikite katika kutatua changamoto zinazogusa jamii ikiwemo ya ujenzi wa matundu ya choo.
Mjumbe wa kamati ya shule Solomon Mukhenyi alikiri kuwepo kwa mvutano wa itikadi za kisiasa unaokwamisha ukamilishaji wa matundu hayo ya vyoo huku mwenyekiti wa kitongoji cha Kimbiji ambaye ana kaimu nafasi ya mwenyekiti wa kijiji Jacob Mwantandu akiahidi kuwashirikisha wananchi kuhusu ujenzi huo ili ukamilike kwa muda uliopangwa.
Akitoa maelezo ya ujenzi huo afisa ufundi wa halmashauri hiyo Salum Kidesu alisema kulingana na tathimini ya ujenzi waliyofanya waliona gharama za kujenga matundu ya vyoo 20 kwa ajili ya shule hiyo ni shilingi 17,000,000.

Kutokana na hamasa iliyotolewa diwani wa Kata ya Ikungi Abel Nkuwi aliahidi kuchangia shilingi  200,000 na mkazi mmoja Athuman Labia akiahidi kutoa mbuzi na wajumbe wa serikali ya kijiji kasimu Nkhambi na Jumanne Hussein wakiahidi kusimamia ujenzi huo ukamilike baada ya kuondoa tofauti zao za kisiasa.
 

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania