CURRENT NEWS

Wednesday, April 5, 2017

DC SANGA -MZAZI ASIYEPELEKA MTOTO WAKE SHULE HADI SASA KUKIONA

 Wakazi wa kata ya Njianne na wanaCCM wakisikiliza jambo wakati mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga akizungumza
 Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mkuranga Abihudi Shilla akizungumza 
 Katibu wa siasa na uenezi mkoani Pwani, Dk. Zainab Gama akiongea jambo huko kata ya Njianne wilaya ya Mkuranga.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga akizungumza na wananchi, kata ya Njianne wilayani hapo. (picha na Mwamvua Mwinyi)  

Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga

MKUU wa wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Filberto Sanga amewataka wazazi ambao watoto wao wamefaulu kuingia kidato cha kwanza kuwapeleka shule mara moja, na atakaebainika kukaa na mtoto nyumbani atakiona. 

    Aidha amewataka wazazi wenye
    watoto waliofikia umri wa kuanza         darasa la kwanza kwenda kuwaandikisha bila kufanya ajizi. 
Amesema kuanzia sasa ataambatana na timu yake, kupita kuhakiki kijiji hadi kijiji na endapo atakutwa mtoto hajapelekwa shule mzazi wake atafikishwa mahakamani. 

Sanga alisema msimamo huo,wakati akizungumza katika kata ya Msonga, Magawa, Njianne, Kitomondo na Mwarusembe wilayani hapo kwenye mikutano ya ndani iliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani.

Alieleza licha ya serikali kuagiza elimu kutolewa bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne lakini wapo wazazi mpaka sasa wanaoshindwa  kuwapeleka shule watoto wao kwa sababu zisizoeleweka.

Sanga alisema atalivalia njuga suala hilo hadi hapo atakapohakikisha watoto hao wameripoti mashuleni.  

Alifafanua kwamba sekta ya elimu haina utani hata kidogo na ni haki ya mtoto  .

Sanga alibainisha kwamba, watoto bila kuwa na elimu wilaya hata mkoa na taifa haitojikomboa.

"Asilimia 80 ndio walioripoti mashuleni wengine wapo majumbani ,hivyo wazazi wawe na mwamko wa elimu ili kuwakomboa  watoto wao”
“Serikali inachangia vitu vyote vya msingi ,sioni sababu ya mzazi kukaa na bila elimu, atakaekaidi agizo hili afikishwe mahakamani”alisisitiza Sanga. 
Kwa upande wake,katibu wa siasa na uenezi CCM mkoani Pwani, Zainab Gama, aliwataka wazazi kuwalinda na kuwalea watoto kwa umoja kwani mtoto wa mwenzio ni wako.

Alisema vijana wengi wanaharibika kutokana na kuiga maadili ya nchi za nje na kushawishiana.

Gama aliiomba jamii kukemea watoto na vijana ambao wanakiuka mila, desturi na maadili ya nchi bila kuwaonea aibu.

Nae katibu wa CCM wilaya ya Mkuranga, Abihudi Shilla alisema anaunga mkono suala la watoto kufikishwa shule kwa wakati kwa kuwa anatambua umuhimu wa elimu.

 Shilla anasema, endapo  watu wanachangia harusi na sherehe kuna kila sababu ya kuipa kipao mbele elimu ili kuwajengea watoto msingi bora katika maisha yao ya baadae. 

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania