CURRENT NEWS

Friday, April 14, 2017

KIWANDA CHA PRAYOSE CHAIBIWA MALI NA FEDHA VYENYE THAMANI YA MIL. 25/WANNE WAJERUHIWA KWA NONDO

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

KUNDI la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia kiwanda cha prayose wilayani Kisarawe mkoani Pwani na kupora fedha na mali zenye thamani ya mil. 25.

Kati ya vitu vilivyoporwa ni pamoja na fedha taslimu sh mil. 18,laptop mbili za mil. mbili na simu 14 zenye gharama ya mil. tano. 

Aidha katika tukio hilo watu wanne wenye asili ya kihindi wamejeruhiwa kwa kupigwa na nondo kwenye maeneo mbalimbali ya miili yao. 

Kufuatia tukio hilo jeshi la polisi mkoani Pwani, linawashikilia walinzi waliokuwa zamu kwa mahojiano. 

Kamanda wa polisi mkoani hapo, kamishna msaidizi mwandamizi, Onesmo Lyanga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, april 13 majira ya saa 7 usiku  .

Alisema huko maeneo ya kiwanda hicho, kundi la watu zaidi ya sita wakiwa na mapanga na marungu walikivamia na kuwafunga kamba walinzi wawili waliokuwa zamu kisha kuingia ndani ya kiwanda na kujeruhi wahindi wanne. 

Kamanda Lyanga alieleza, licha ya kuwajeruhi watu hao ,waliweza kuwafunga kwa kamba wafanyakazi waliokuwa wakiendelea na uzalishaji kiwandani ambapo  walifanikiwa kupora mali na fedha. 

Alitoa rai kwa wafanyabiashara kuacha kuhifadhi kiwango kikubwa cha fedha ndani na badala yake fedha hizo wakazihifadhi kwenye taasisi za kifedha -bank kwa usalama zaidi. 

"Wafanyabiashara wajitambue kwani kuweka fedha ndani, kwenye kampuni ni risk "

"Kufuatia suala hilo lilivyo tunawashikilia walinzi wa kampuni hiyo kwa uchunguzi zaidi "alisema. 

Kamanda Lyanga aliomba ushirikiano kwa jamii kulisaidia jeshi hilo mara watakapobaini watu waliofanya tukio hilo. 

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania