CURRENT NEWS

Saturday, April 29, 2017

KUONGEZEKA MIVUTANO BAINA YA MAREKANI NA RUSSIA KUHUSU SYRIA

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika Alkhamisi jioni katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, kimejikita kwenye hali ya kibinadamu katika nchi ya Syria iliyoharibiwa vibaya na vita.
Katika kikao hicho, Nikki Haley, mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ametaka kuongezwa mashinikizo dhidi ya Russia. Amesisitiza kuwa, inabidi mashinikizo yote yaelekezwe kwa Russia kwani nchi hiyo ndiyo pekee inayoweza kuondoa hali hiyo.
Kwa upande wake, Petr Iliichev, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amemjibu mjumbe huyo wa Marekani kwa kusema, vitendo na miamala miovu ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani nchini Syria ndiyo inayoshadidisha hali mbaya ya kibinadamu nchini humo na hazifanyi juhudi zozote za kuboresha hali hiyo. Kikao cha Baraza la Usalama kwamba mara nyingine kimeshuhudia mivutano baina ya Marekani na Russia kuhusiana na Syria.
Serikali ya Marekani hivi karibuni ilifanya shambulizi la makombora dhidi ya wanajeshi wa Syria huko Homs na hivyo kuonesha kwa uwazi namna ilivyo na msimamo wa kiuadui dhidi ya serikali ya Syria na hivi sasa imeamua kuishambulia kwa maneno Russia ikidai kuwa Moscow ndiyo inayokwamisha utatuzi wa mgogoro wa Syria. Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, vitendo vya Marekani na waitifaki wake wa nchi za Kiarabu, kieneo na za Kiarabu huko Syria vinaonesha kwamba Wamagharibi ndio wahusika wakuu wa mateso waliyo nayo hivi sasa wananchi wa Syria. 
Petr Iliichev, mjumbe maalumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa
Hata katika wakati huu wa urais wa Donald Trump nchini Marekani ambaye wakati wa kampeni zake za uchaguzi alidai kuwa atabadilisha siasa za nchi yake kuhusiana na Syria na ataelekeza nguvu zake katika kupambana na kundi la kigaidi la Daesh, amebadilisha kikamilifu msimamo wake na anaendeleza yale yale yaliyokuwa yakifanywa na serikali iliyopita ya Marekani shabaha kuu ikiwa ni kutaka kuipindua serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wenyewe wa Syria.
Nchi za Magharibi na hususan Marekani zinaona namna Russia ilivyofanikiwa katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi nchini Syria na haziwezi kuizuia Moscow kuendelea na siasa zake hizo nchini Syria, hivyo zimeamua kuendesha vita vya kisaikolojia na kipropaganda na kushadidisha mashinikizo ya kisiasa na kidiplomasia dhidi ya Russia ili kuifanya Moscow angalau ipunguze uungaji mkono wake kwa serikali ya Syria.
Uhakika huo unathibitishwa pia na Valery Semerikov, Kaimu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mkataba wa Usalama wa Kijamii (CSTO) akazilaumu nchi za Magharibi kwa kuwatelekeza wananchi wa Syria na kufanya njama za kuikwamisha Russia katika juhudi zake za kutatua mgogoro wa nchi hiyo. Amesema, mashambulizi ya silaha za kemikali katika nchi za Iraq na Syria yamepangwa na kufanywa na makundi ya kigaidi lakini nchi za Magharibi zimegeuza uhakika wa mambo na kuituhumu Damascus kuwa ndiyo iliyofanya mashambulizi hayo ili kupotosha fikra za walimwengu kuhusiana na vita dhidi ya ugaidi na kupunguza umuhimu wa vita vinavyoendeshwa na Russia na waitifaki dhidi ya makundi ya kigaidi huko Syria.
Wanajeshi wa Uingereza ndani ya ardhi ya Syria, wameingia nchini humo bila ya idhini ya serikali ya wananchi wa nchi hiyo
Vile vile alielezea wasiwasi wake wa kugeuzwa vita vya Syria kutoka katika suala ya vita vya eneo la Mashariki ya Kati na kuwa vita vya pande zote vinavyotumia silaha za mauaji ya umati. Matamshi ya kiongozi huyo mwandamizi wa jumuiya kubwa ya kiusalama ya CSTO yanaonesha namna Russia ilivyo na wasiwasi wa matokeo mabaya ya siasa za nchi za Magharibi kuhusiana na Syria. Cha kusikitisha ni kwamba nchi za Magharibi na waitifaki wao haziachi kuchukua hatua yoyote ile hata ya kuuunga mkono mashambulizi ya silaha za kemikali yanayofanywa na makundi ya kigaidi, alimradi tu yafanikishe malengo yao haramu nchini Syria.
Hata hivyo kichekesho kikubwa zaidi ni kuziona nchi hizo hizo za Magharibi ikiwemo Marekani, zinalilaumu jeshi la Syria kuwa eti ndilo lililotumia silaha hizo kabla ya hata kufanyika uchunguzi wowote kuhusua suala hilo. Inaonekana lengo la nchi za Magharibi ni kuishinikiza serikali ya Damascus na waitifaki wake na kujaribu kuzuia mafanikio yake katika kupambana na magaidi na kuwalinda wananchi wa Syria.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania