CURRENT NEWS

Thursday, April 27, 2017

KUPAMBA MOTO TENA MIKWARUZANO KATI YA KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

Sambamba na kuwadia maadhimisho ya mwaka wa 85 wa kuasisiwa jeshi la Korea Kaskazini na kukaribia kutimia siku 100 tangu Donald Trump atawazwe kuwa rais wa Marekani mikwaruzano ya kisiasa baina ya Pyongyang na Washington imeshtadi na kuzidi kupamba moto.
Katika mazungumzo aliyofanya na mabalozi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Rais Donald Trump wa Marekani amesema siasa zinazotekelezwa hivi sasa na umoja huo kuhusiana na Korea Kaskazini hazikubaliki na akadai kwamba nchi hiyo ni hatari kubwa kwa dunia. Trump aidha amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liiwekee vikwazo vipya Pyongyang. Wakati huohuo Nikki Haley, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa ameshawapa taarifa wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba wakati umeshawadia kwa Washington kuchukua hatua za kivitendo kukabiliana na Korea Kaskazini.
Nikki Haley, balozi wa Marekani UN
Hayo yanajiri huku baadhi ya duru za habari zikizungumzia uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya jaribio la sita la silaha za atomiki kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 85 wa kuundwa jeshi la nchi hiyo. Uwezekano huo umezidi kuifanya hali ya mgogoro inayotawala katika eneo la Mashariki ya Asia iwe mbaya zaidi. Marekani imeonya kuwa itachukua hatua kukabiliana na kitendo hicho, na kwamba si hasha ikaamua hata kupigana vita na Korea Kaskazini. 
Nayo Pyongyang inasisitiza kwamba, kuzidi kujizatiti kijeshi Marekani kandokando ya Peninsula ya Korea, kutumwa manowari mpya za nchi hiyo katika eneo hilo na kauli za mara kwa mara za vitisho zinazotolewa na Trump vimezidi kuifanya hali ya mambo iwe mbaya zaidi.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un (kulia) na Trump 
Inavyoonyesha, kwa kuzidi kukaribia siku 100 tangu serikali mpya ya Marekani iingie madarakani, Donald Trump hahisi ni jambo baya kuzusha mgogoro kimataifa na kuzidi kukoleza moto wa hatari ya kutokea vita katika eneo la Mashariki ya Asia ili kuzizubaisha fikra za waliowengi na kuziweka mbali na masuala ya ndani ya Marekani.
 Katika kipindi cha zaidi ya siku 90 zilizopita, Rais huyo wa Marekani amekumbwa na kashfa kadhaa na pia kugonga mwamba katika kutekeleza mengi ya aliyoahidi kabla hajaingia madarakani. Hii ni pamoja na kashfa ya uhusiano wa siri uliokuwepo baina ya watu wake wa karibu na Russia, kushindwa kutekeleza amri yake mpya aliyotoa dhidi ya wahajiri na vilevile kutoweza kuufuta kama alivyoahidi, mpango wa bima ya matibabu ya gharama nafuu maarufu kwa jina la Obamacare. 
Matatizo yote hayo yamezidi kupunguza umaarufu wa Trump mbele ya wananchi wa Marekani. Uchunguzi wa maoni uliofanywa umeonyesha kuwa, kati ya marais wa Marekani walioongoza nchi hiyo tangu baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Donald Trump amekuwa na kiwango cha chini zaidi cha umaarufu na uungaji mkono wa wananchi katika siku 100 za mwanzo za utawala wake. Kuendelea lawama na manung'uniko yanayomwandama rais wa Marekani kutasababisha madhara makubwa kwa mipango ya serikali yake na kwa nafasi ya chama chake cha Republican. 
Kuzuka mgogoro katika sera za nje na kujitokeza Trump kama rais shupavu na jasiri wa kuweza kukabiliana na kile kinachotajwa kama vitisho vya kiusalama dhidi ya Marekani  kunaweza kuugeuza kikamilifu mkondo wa kuporomoka kiwango cha umaarufu wa rais wa nchi hiyo. Na hilo limeshuhudiwa katika wiki chache zilizopita baada ya Trump kutoa amri ya kuishambulia kwa makombora Syria kwa kisingizio cha kutumia silaha za kemikali katika mji wa nchi hiyo wa Khan Sheikhoun, ambapo rais huyo wa Marekani aliungwa mkono ndani na nje ya nchi hiyo.
Manowari za Marekani zikielekea Peninsula ya Korea
Lakini ni wazi kwamba kuanzisha chokochoko za mgogoro dhidi ya Korea Kaskazini kuna tofauti kubwa mno na kufanya hivyo kuhusiana na Syria. Kwa kuwa Syria imetingwa na vita kamili vya muda wa miaka sita vya kukabiliana na magaidi pamoja na muungano wa kijeshi wa maajinabi wa Magharibi na wa nchi za Kiarabu,  nchi hiyo haina uwezo wa kutosha wa kujibu mapigo ya moja kwa moja kwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani. 
Lakini Korea Kaskazini inao uwezo wa kufanya hivyo dhidi ya shambulio lolote la kijeshi la Marekani, kwa kutumia uwezo wake wa makombora na wa silaha za atomiki. Isitoshe, haiwezekani kubariziana kijeshi na Korea Kaskazini bila ya kuwa tayari pia kuikabili hatari ya uwezekano wa kuvaana kijeshi na China ambayo ni muitifaki mkuu wa Pyongyang.  
Mahesabu hayo ya mezani yanavifanya vitisho vya maneno vya mara kwa mara vinavyotolewa na Trump dhidi ya Korea Kaskazini vionekane kuwa havina mashiko kiutekelezaji, isipokuwa kama Rais wa Marekani atakuwa amedhamiria kweli kuanzisha chokochoko za kijeshi ili kuitumbukiza dunia kwenye vita vyengine angamizi katika eneo hasasi la Mashariki ya Asia
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania