CURRENT NEWS

Saturday, April 22, 2017

MAHAFALI YA PILI YA KIDATO CHA SITA YA SHULE YA SEKONDARI WAMA NAKAYAMA YAFANA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete pamoja na viongozi wengine wakiangalia kwa vitendo majaribio ya kiyasansi kutoka kwa wanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya WAMA NAKAYAMA kwenye sherehe za mahafali yao ambapo wanafunzi 45 wamehitimu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete(kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa WAMA Bi.Zakhia Meghji wakiimba wimbo maalumu wa shule ya Sekondari ya WAMA NAKAYAMA wakati wa mahafali ya pili ya kidato cha sita ambapo wanafunzi 45 wamehitimu. 
 Baadhi ya Wanafunzi waliohitimu kidato cha sita katika shule ya sekondari WAMA NAKAYAMA.
Theresia Sanu (kulia)akisoma risala ya wahitimu kwa Mgeni Rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa mahafali ya pili ya kidato cha sita ya shule ya sekondari ya WAMA NAKAYAMA.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye mahafali ya pili ya kidato cha sita ya shule ya Sekondari ya WAMA NAKAYAMA ,ambapo aliwaasa wanafunzi hao 45 kusoma zaidi ili waje kulisaidia Taifa lao.
Mwenyekiti wa WAMA Mama Salama Kikwete akihutubia katika mahafali ya kidato cha sita ya shule ya WAMA NAKAYAMA ambapo aliwataka wanafunzi hao kusoma na kufika juu zaidi.

                                             .................................................................................

             Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewahimiza  wanafunzi kote nchini kupenda kusoma masomo ya Sayansi hasa watoto wa kike ili Taifa liweze kujitosheleza kwa wataalamu wa fani mbalimbali nchini hasa wakati huu ambao Taifa linaelekea kwenye uchumi wa Viwanda.
 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwenye mahafali ya Pili ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wa shule ya sekondari ya WAMA- NAKAYAMA , mahafali ambayo imehudhuriwa na wake wa Marais Wastaafu.


Makamu wa Rais amesema haitapendeza hata kidogo ajira nyingi nchini kuchukuliwa na wataalamu mbalimbali mataifa ya nje hasa kipindi hiki wakati Serikali inahimiza ujenzi wa viwanda hivyo amesisitiza wanafunzi wajikite kwenye kusoma masomo ya sayansi ili taifa liweze kujitosheleza kwa ajili ya manufaa ya maendeleo ya taifa.

Amesema katika kuhakikisha taifa lipata wanasayansi wengi, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa maabara na kununua vifaa vya maabara ili kuhamasisha wanafunzi wengi zaidi kupenda kusoma masomo ya sayansi kote nchini.


Makamu wa Rais pia amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Tano inakusudia kuimarisha ufundishaji wa masomo ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano –TEHAMA- katika shule za Sekondari na kujenga maabara za kompyuta nia ikiwa ni kuongeza wataalamu wa fani hiyo nchini.

Kuhusu mila na desturi kandamizi kwa wanawake na wasichana zilizopo kwenye baadhi ya jamii nchini, Makamu wa Rais ameitaka jamii kukomesha mila hizo na iwashirikishe wanawake katika mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi kwani watakuwa ni chachu ya maendeleo katika jamii husika.


“Wote tunajua wanawake ni chachu na kiungo muhimu katika maendeleo ya jamii, Taifa na Dunia kwa ujumla hivyo ni wajibu wa jamii kushirikisha wanawake katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo kote nchini” amesisitiza Makamu wa Rais.


Makamu wa Rais pia ameipongeza Taasisi ya Wanawake na Maendeleo – WAMA- kwa kujenga shule Mbili za Sekondari na kusomesha watoto wanaotoka kwenye familia maskini na yatima na kusema huo ni mfano wa kuingwa na wadau wengine wa maendeleo katika kusaidia kundi hilo ili watoto wanaotoka kwenye familia maskini nao waweze kuapata elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya baadae.

Kuhusu changamoto zinazoikabili shule ya WAMA – NAKAYAMA, Makamu wa Rais ameahidi kushughulikia changamoto hizo ikiwemo uhaba wa maji, ubovu wa barabara kuelekea kwenye shule hiyo na tatizo la uhaba wa mabweni

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WAMA na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mama SALMA KIKWETE amesema aliamua kuanzisha taasisi hiyo ambayo inamiliki shule Mbili mpaka sasa ili kusaidia watoto wa maskini na yatima kupata elimu bure ambapo mpaka sasa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaliohitimu katika shule hizo ambao wamejiunga na masomo ya elimu ya juu.

Mama Salma Kikwete ameshukuru ushirikiano mkubwa anaopata kutoka Serikalini unaolenga kuhakikisha shule zinazoendeshwa na taaisisi hiyo ikiwemo ya Wama – Nakayama zinafanya vizuri.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania