CURRENT NEWS

Friday, April 14, 2017

MAREKANI YATUMIA BOMU KUBWA ZAIDI KUSHAMBULIA IS

MOAB BOMB
Jeshi la Marekani kwa mara ya kwanza limewashambulia wapiganaji wa kundi la Islamic State kwa kutumia bomu kubwa lisilokuwa la nyuklia, kuwahi kutumiwa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani, katika vita.
Bomu hilo aina ya GBU-43 ambalo limetumika kutekeleza shambulio hilo, kipimo chake cha nguvu kilichotumika kinalingana sawa na tani 11 za TNT, na ambalo pia hujulikana kama ''Mama wa mabomu yote'' lilipigwa katika mapango yanayotumiwa na wapiganaji wa Islamic State kujificha katika jimbo la Nangarhar, mashariki mwa Afghanistan.
Akielezea kulipuliwa kwa bomu hilo ardhini Gavana katika Wilaya ya Achin jimboni humo, Esmail Shinwari amesema ni kama vile miale mikali ilimeza eneo hilo.
Mkuu wa kikosi cha jeshi la Marekani nchini Afghanistan, Jenerali John Nicholson amesema bomu hilo lilikuwa ni zana sahihi kutumika kuendeleza kasi ya kupambana na waislamu hao wenye itikadi kali.
Akitoa taarifa Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sean Spicer amesema tahadhari zilichukuliwa kupunguza athari kwa raia kufuatia shambulio hilo.
Naye Msemaji wa Ofisi ya Rais ya Afghan amesema shambulio la bomu hilo litasababisha madhara makubwa.
Lakini kwa upande wake Rais wa zamani wa Afghan Hamid Karzai amelaani matumizi ya silaha hizo na kusema sio kitendo cha ubinadamu.
Ameishutumu Marekani kwa kuitumia Afghanstan kama eneo la majaribio na kuongeza kuwa ni juu ya wa Afghan wenyewe kuizuia Marekani kufanya hivyo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania