CURRENT NEWS

Thursday, April 13, 2017

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YAFAFANUA HATMA YA UBUNGE WA SOPHIA SIMBATume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuutarifu Umma kuwa; kwa mujibu wa Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa; kufuatia Mbunge wa Viti Maalum, SOPHIA MNYAMBI SIMBA kufukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi tarehe 11 Machi, 2017 kiti cha Mbunge huyo wa Viti Maalum Wanawake kwa tiketi ya CCM kiko wazi.
         Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili mtu ateuliwe au achaguliwe katika nafasi ya Ubunge ni lazima awe mwanachama aliyependekezwa na Chama chake husika cha Siasa.
         Kwa kuwa Ndg. SOPHIA MNYAMBI SIMBA amefukuzwa uanachama wa Chama kilichomdhamini, Ibara ya 67 (2) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaelekeza kuwa Mbunge huyo amepoteza sifa za kuteuliwa au kugombea Ubunge.
         Kutokana na kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge wa Viti Maalum, taratibu za kujaza nafasi hiyo zinaendelea kwa kuzingatia kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.


Jaji (R) Semistocles Simon Kaijage
Mwenyekiti
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

12  Aprili, 2017
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania