CURRENT NEWS

Saturday, April 29, 2017

WATUMISHI HEWA PWANI WARUDISHA MIL.81.245 WALIZOLIPWA MISHAHARA

 Mkuu wa Dawati la sheria na mashtaka TAKUKURU mkoani Pwani, John Sang'wa akitolea ufafanuzi jambo kwa waandishi wa habari.

Kamanda wa TAKUKURU Pwani, Suzan Raymond, akizungumza katika mkutano wa kutoa taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha July 2016-March 2017.
 (picha na Mwamvua Mwinyi) 

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KAMANDA wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU)mkoani Pwani,Suzan Raymond,ameeleza kuwa taasisi hiyo imeokoa kiasi cha sh.mil 81.245,katika kipindi cha July 2016-March-2017.
Amesema fedha hiyo imetokana na watumishi hewa waliobainika mkoani hapo,ambao walikuwa wakilipwa mishahara kinyume na utaratibu.
Aidha kamanda Suzan amesema,idara ya serikali za mitaa hasa  katika mamlaka za watendaji wa vijiji/mitaa/kata na polisi bado zinaendelea kutafunwa na malalamiko yanayohusiana na rushwa.
Akitoa taarifa ya utekeleza kwa kipindi cha miezi Tisa,alisema kwa kuzingatia maagizo kutoka mamlaka za juu,watumishi hao walitakiwa kulipa fedha zote walizokuwa wakilipwa wakati wa utumishi tata.
Hata hivyo,alisema mafaili mawili ya watumishi 16 yamepelekwa makao makuu ya TAKUKURU kisha wataomba kibali kwa DPP kwa ajili ya kufungua kesi kwa wale watakaobainika kuhusika na ubadhilifu wa fedha .
Kwa mujibu wa Suzan,maafisa utumishi hawahusiki moja kwa moja kusababisha watumishi hewa kutokana na kuingiliana kwa majukumu baina yao na wakuu wengine wa idara ikiwemo walimu wakuuu.

Kamanda Suzan alibainisha,katika kipindi hicho,ofisi hiyo ilipokea malalamiko 363 kati ya hayo malalamiko 252 yanahusiana na vitendo vya rushwa na uchunguzi wake unaendelea.
Alisema malalamiko 98 hayahusiani na vitendo vya rushwa ,ambapo walalamikiaji walishauriwa na wengine walisaidiwa kwa kuwasiliana idara husika kwa lengo la kutatuliwa kero zao.
“Idara inayoongoza kwa malalamiko ya vitendo vya rushwa ni serikali za mitaa kwa malalamiko 135 hasa mamlaka za watendaji wa vijiji/mitaa na kata ikifuatiwa na polisi yenye malalamiko 44”
Kamanda Suzan alifafanua ,mahakama malalamiko 43,idara ya afya 26,ardhi 24,elimu 17,sekta binafsi malalamiko 17,baraza la ardhi 05,ushirika 11,maliasili 02 na kilimo 02.
Alisema malalamiko kwenye idara ya misitu 11,habari 01,TASAF 01 ,fedha 01,viwanda 01,mgambo 01,ujenzi 05,maji 05,madini 03,serikali kuu 02,uvuvi 02,TAMISEMI 01,TANAPA 01 na kilimo 01.
Kamanda huyo alisema taasisi hiyo,imeshafungua kesi mpya tatu katika mahakama ya wilaya na mkoa pia mkoa una kesi nne zinazoendelea kusikilizwa,na wanatarajia kufuangua kesi kumi.
Kamanda Suzan alisema ,wanaendelea na majukumu yake kwa kuelimisha umma,kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazohusiana na vitendo vya rushwa na uendeshaji wa mashtaka pamoja na kufanya uchambuzi wa mifumo .
“Lengo ni kubaini mianya ya rushwa na kutoa ushauri wa namna ya kuiziba katika taasisi na idara mbalimbali kimkoa. takiwa kuzirejesha kwa utaratibu uliokuwepo”alisema.
Nae mkuu wa dawati la sheria na mashtaka TAKUKURU mkoani Pwani,John Sang’wa ,alielezea kuwa,wanatarajia kufikisha mafaili ya uchunguzi wa watumishi hewa ambao tayari wamerejesha walizolipwa kama mshahara ,kwa mwendesha mashataka mkuu wa serikali( DPP).
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania