CURRENT NEWS

Monday, April 10, 2017

ROMA AFUNGUKA MBELE YA MWAKYEMBE

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza kwenye mkutano wa Msanii Roma na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Maelezo jijini Dar es Salaam.
Msanii Roma Mkatoliki akionyesha sehemu ya mkono wake uliojeruhiwa na watekaji kwenye mkutano wa waandishi wa habari.

                              ..........................................................................
    Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb) leo Jumatatu tarehe 10 Aprili, 2017 amekutana na msanii wa kizazi kipya Roma Mkatoliki kwenye ofisi ndogo za Wizara, Habari Maelezo, Dar es Salaam. Mhe. Mwakyembe aliambatana na Mkurugenzi wa Habari Maelezo pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania. Mhe. Mwakyembe ametoa pole kwa Msanii Roma ambaye yeye na wenzake watatu walitekwa na watu wasiojulikana na amesisitiza nia njema ya Serikali katika kulinda watu na mali zao.

 Aidha, Mhe. Mwakyembe amewahakikishia wasanii ushirikiano katika masuala mbalimbali yanayohusu tasnia yao. Vilevile Mhe. Mwakyembe amewaasa wasanii wa muziki kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwenye utunzi na uimbaji wa nyimbo zao ili waweze kufanikiwa kibiashara na kuepuka mikwaruzano baina yao wenyewe  na wakati mwingine na Serikali. Pamoja na hayo, Mhe. Mwakyembe amewashauri wananchi kutopotosha ukweli wa suala hilo la kutekwa kwa msanii Roma kwa kutoa taarifa za uchonganishi na zisizo na ukweli na wasubiri taarifa kamili kutoka kwa Jeshi la Polisi baada ya upelelezi kukamilika, "Ndugu waandishi na wananchi nawaasa kuacha kupiga ramli kwenye suala hili la kisayansi na kiupelelezi" alisititiza. 

Kwa upande wake, Msanii Roma ameishukuru Serikali kwa kuwa karibu na wasanii na kwa jinsi ilivyolishughulikia suala lake. Roma pia amewashukuru viongozi Serikali katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa jitihada walizofanya kuhakikisha anapatikana akiwa salama. Kwa namna ya pekee Roma amewashukuru pia wasanii wenzake, mashabiki wa muziki na Watanzania kiujumla kwa kuwa pamoja naye na familia yake.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania