CURRENT NEWS

Wednesday, May 31, 2017

CHALINZE YAIANGUKIA SERIKALI BAADA YA FAGIO LA KUBAINI VYETI FEKI

 Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze ,Said Zikatimu akizungumza katika baraza la madiwani 
Madiwani na watendaji wa halmashauri ya Chalinze wakisikiliza jambo wakati wa kikao cha baraza la madiwani lililofanyika Lugoba .(picha na Mwamvua Mwinyi )

HALMASHAURI ya Chalinze,Bagamoyo ,mkoani Pwani imeiomba serikali kupeleka watumishi katika idara ya afya na elimu ,mara baada ya utaratibu wa uhakiki kukamilika ,ili kuziba pengo la upungufu wa watumishi 42 waliokumbwa na adha ya vyeti feki katika halmashauri hiyo.

Aidha halmashauri hiyo ,imefanikiwa kutimiza malengo yake sita ndani ya kipindi cha miezi Tisa ,ikiwemo kuinua mapato yake ya ndani.

Hayo yaliyasemwa na mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze, Said Zikatimu , wakati akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani,huko Lugoba .

Alielezea kuwa ,wameinua mapato hayo kutoka kiasi cha sh .mil 130 hadi kufikia sh.mil 390 sawa na asilimia 120 na kuwa ya kwanza kimkoa.

Zikatimu alisema ,wameimarisha usimamizi wa makusanyo yao mbalimbali .

Alibainisha kwamba ,mbali ya hilo ,katika kipindi hicho wameshakopesha sh .mil 180 kwa vikundi vya wanawake na vijana 58 vilivyopo kwenye kata za halmashauri hiyo .

Hata hivyo Zikatimu ,alieleza wanalipa wenyeviti wa vijiji na vitongoji sh .30,000 kila mwezi kutoka katika mapato hayo .

"Wenyeviti hawa wanafanya kazi kubwa hivyo tukaona ni vyema kuwalipa japo kiasi hicho kidogo cha fedha " alisema.

Mwenyekiti huyo ,alisema pia kwa sasa hakuna mwananchi anaetozwa fedha za mafuta ya magari ya wagonjwa kwenye vituo vya afya baada ya halmashauri kuamua kutenga fungu la fedha ya mafuta kwenye vituo vya afya .

Zikatimu alisema ,katika miradi ya maendeleo wametenga asilimia 60 ya mapato yao ambayo hufanyia mambo mbalimbali kama kujenga nyumba za walimu ,vyoo ,kununua matrekta na mengineyo .

Kwa mujibu wake ,wanatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ,kwa vitendo na wameomba wananchi washiriki kulipa kodi na ushuru pasipo kukwepa .

Akizungumzia ishu ya vyeti feki ilivyowaathiri,Zikatimu ,,alisema watumishi 42 wamekubwa na adha hiyo kati yao 26 ni walimu ,watatu ni watendaji wa vijiji na waliobakia ni idara ya afya .

Alisema zoezi hilo limeathiri na halmashauri hiyo kwani awali kulikuwa na mapungufu ya walimu na watumishi wa afya sasa kwa ongezo lililotokea changamoto ya upungufu wa huo imekuwa kubwa.

"Wodi za uzazi akina mama wajawazito wanapata shida ,wagonjwa wa dharura wanapata kero ,na wanafunzi wamekuwa wakikosa kusoma kama inavyotakiwa " alisema Zikatimu .

Zikatimu aliipongeza serikali kwa kubaini watu waliokuwa wakila mshahara kinyume na taratibu ambapo ameiomba ,ione mapungufu yaliyoongezeka ili kupunguza ama kuondoa upungufu uliojitokeza .

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania