CURRENT NEWS

Sunday, May 28, 2017

HALMASHAURI KUU YA CCM PWANI YALAANI WATU 16 KUTISHIWA KUUAWA/MAUAJI KIBITI


Katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM )mkoani Pwani, dk.Zainab Gama ,aliyeketi katikati akitoa tamko la halmashauri kuu ya CCM mkoani humo kulaani vitendo vya mauaji ,wa kulia ni mwenyekiti wa UVCCM mkoani Pwani, Mohammed Nyundo.
 Katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM )mkoani Pwani, dk.Zainab Gama ,akizungumza baada ya kikao cha halmashauri kuu ya CCM mkoani hapo (picha na Mwamvua Mwinyi )

Na Mwamvua Mwinyi ,Pwani

HALMASHAURI kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),inasikitishwa kupokea taarifa ya baadhi ya viongozi wa serikali na wanachama wake 16 kutishiwa kuuawa huko wilaya ya Kibiti,Rufiji na Mkuranga .

Aidha imeeleza hadi sasa viongozi wa serikali 14 na wanaCCM 13 na kuweka idadi ya 27 wameuawa katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo vitendo vya mauaji vimetokea .

Mbali ya hilo ,watu saba walijeruhiwa na kunusurika kifo kati yao wanne ni wanaCCM.

Kutokana na hali hiyo ,wajumbe wa halmashauri hiyo ,may 27 walitoa tamko la kulaani vikali mauaji yaliyotokea katika maeneo hayo .

Katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoani Pwani ,Zainab Gama ,alisema wametaarifiwa kutishiwa kuuawa kwa viongozi 16 kati yao 10 wakiwa wana CCM .

Kwa mujibu wake ,kuendelea kwa matukio hayo kunasababisha watu wajenge hofu ya kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi.

"Watu wanatishiwa hadi misibani ,wanafunga maduka na kuingia majumbani saa 12 kwa kuogopa ,haya sio maisha mazuri lazima tumuogope mungu" alisema Zainab .

Alielezea ,watu hawana hatia ,lakini wamekuwa wakitishiwa kuuawa bila kujua kosa lao .

Zainab alisema ,watanzania wawe wazalendo ,wawe na hofu ya mungu na kupendana ili kuishi kwa amani .

Alibainisha ,CCM ina imani kubwa na serikali chini ya Rais dk .John Magufuli ,na jeshi la polisi inavyoendelea kupambana na vitendo vya mauaji .

"Tunaimani kwa hatua iliyofikia hadi sasa na juhudi zinazofanyika ili kuhakikisha hali hiyo inamalizika " alisema .

Pamoja na hayo ,aliipongeza serikali kwa kuanzisha kanda maalum ya kipolisi 

Zainab aliwaomba wananchi na wanaCCM wasitishwe wala kuogopa ama kurudi nyuma juu ya matukio hayo kwa kuwa serikali inalishughulikia suala hilo.

Aliwasihi wananchi na wanachama kushirikiana na Polisi na serikali kuwafichua watu wanaowatilia shaka .

Alipoulizwa kuhusiana na ombi la wananchi la kuomba vyama vya siasa ikiwemo  CUF na CCM kukaa meza moja kupambana na jambo hilo linaloonekana harufu ya itikadi za kisiasa ."Zainab alijibu ni suala la ngazi ya juu hawezi kulisemea .

Nae mwenyekiti wa jumuiya wa vijana ya chama cha mapinduzi (UVCCM),Mohammed Nyundo ,alibainisha jukumu la ulinzi ni la kila mmoja hivyo wananchi watambue umuhimu wa kuwataja watu wasio wema ili wachukuliwe hatua za kisheria .

Alieleza inasikitisha kuona jamii inashindwa kufanya shughuli za kiuchumi na kusababisha kuyumba kimaendeleo .

Nyundo ,aliwasihi wanaCCM kuondoa shaka kwenye nafsi zao na kusimamia chama kwani hakuna refu lisilo na ncha .

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania