CURRENT NEWS

Thursday, May 25, 2017

JAFO:'UTENDAJI HUU NDIO UNAOTAKIWA'

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Kongwa na Wananchi wa Kijiji cha Mkutani katika ukaguzi wa daraja la eneo hilo ambalo ujenzi wake umekamilika.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua ujenzi wa daraja la Kijiji cha Mkutani.

Muonekano wa Daraja la Kijiji cha Mkutani kwasasa baada ya kukamilika ujenzi wake.

Wananchi wa Kijiji cha Mkutani wakipita katika Daraja lao ambalo awali lilivunjika kutokana na Mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2013.

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua maeneo mbalimbali ya Daraja la Mkutani.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Kongwa na Wananchi wa Kijiji cha Mkutani katika ukaguzi wa daraja la eneo hilo.
Daraja la Mkutani                             Wananchi wa Kijiji cha Mkutani wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo alipokuwa akikagua ujenzi wa daraja la Mkutani.
 ............................................................................................................................
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo ameridhishwa na utekelezaji wa maagizo ya serikali yanayotolewa kwa watendaji wa serikali kwa ngazi za halmashauri.

Jafo aliyasema hayo leo mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi ya ujenzi wa daraja katika kijiji cha Mkutani wilaya ya Kongwa lilogharimu kiasi cha Sh.Milioni 195.

Ukaguzi huo wa daraja ulitokana na maagizo aliyoyatoa Mwezi Februari mwaka huu baada ya kutembelea na kukuta kukiwa na kasi ndogo ya ujenzi wa daraja hilo.

Kutokana na hali hiyo,  Jafo alitoa agizo la kujengwa daraja hilo usiku na mchana katika ubora unaotakiwa ili kuwaondolea wananchi kero kubwa ya kukosa daraja linalowaunganisha na barabara ya Makao makuu ya Wilaya.

Alitaka ujenzi wa daraja hilo ukamilike ndani ya miezi mitatu iliyokuwa imebaki kwenye mkataba wa ujenzi huo.
Akizungumza leo mara baada ya kukagua, Jafo alisema ujenzi wa daraja hilo umekamilika  na kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa na timu yake kwa kutekeleza maagizo yake ndani ya muda na kuleta ukombozi kwa wananchi.

Jafo aliwataka watendaji wa serikali za mitaa katika halmashauri zote nchini kuiga mfano huo wa uwajibikaji.

Wananchi wa kijiji hicho waliipongeza serikali mbele ya Naibu Waziri Jafo kwa kuwajengea Daraja ambalo lilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo yao.

Walisema kukatika kwa daraja hilo kulisababisha kukosekana kwa mawasiliano ya barabara kati yao na makao makuu ya wilaya huku wakidai kuwa walikuwa wakipata adha kubwa hasa kipindi cha masika.

Mmoja wa wananchi hao ambaye ni Mwenyekiti wa  kitongoji cha Mkutani,Walesi Nzijila aliishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hilo.

Alisema wakati wa masika wananchi wenye mashamba upande wa pili wa daraja walishindwa kuvuka kwenda mashambani na hata wanafunzi walishindwa kuvuka kwenda shule.

Alisema Daraja hilo awali lilisombwa na mafuriko na kusababisha kwa zaidi ya miaka minne wananchi wa vijiji na vitongoji jirani vya Mkutani kukosa mawasiliano.

Ujenzi wa Daraja hilo ulianza Agosti 2016 baada ya kuvunjika mwaka 2013 kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kipindi hicho.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania