CURRENT NEWS

Thursday, May 11, 2017

RC NDIKILO AMALIZA ZIARA YAKE KIMKOA NA KUSISITIZA MAMBO MAKUU MANNE


Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, akiwa ametembelea shamba la mfano la zao la biashara la korosho lililopo Ruvu JKT, wilayani Kibaha. (picha na Mwamvua Mwinyi) . …………………………………………………………………..

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,amemaliza ziara yake ya kutembelea wilaya sita kimkoa,ambapo amehimiza mambo makuu manne ikiwemo ulinzi na usalama,uwekezaji,kilimo cha matunda na korosho.

Aidha amekemea migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu na wengine kujeruhiwa pasipo sababu za msingi.

Akimaliza ziara yake wilayani Kibaha,mhandisi Ndikilo,alieleza mkoa wa Pwani una viwanda vitatu vikubwa vya kusindika matunda kwa sasa ambavyo endapo wakulima watavitumia watanufaika kwa kiasi kikubwa.

Alisema,kiwanda cha Bakhresa ambacho kipo Mwandege -Mkuranga kimeshaanza kazi na kile cha Elven Agri co.ltd kilichopo kata ya Mapinga -Bagamoyo huku cha Sayona kinachojengwa kata ya Mboga kikiwa kwenye hatua za mwisho za ujenzi.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kiwanda cha kusindika matunda cha Bakhresa kina uwezo wa kusindika tani 350 za matunda kwa siku na uwekezaji wake umegharimu sh.bil.261.

Mhandisi Ndikilo alisema uwekezaji wa viwanda hivyo ni mkubwa na utawatengenezea kipato na soko wakulima wa matunda .

“Niwasihi wakulima wa mkoa wa Pwani na mikoa mingine kulima kwa bidii maembe,nyanya,mananasi,mapeasi,pilipili “

“Sio tu mlime kwa kilimo chetu tulichokizoea ,hapana kwasasa inabidi twende na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa kwa kutumia mbegu,pembejeo bora na mpalilie na kutumia madawa ili kupata matunda yatakayouzika”alifafanua.

Hata hivyo mhandisi Ndikilo aliwaomba wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kukimbilia kuwekeza mkoani Pwani kwani unaelekea kuwa ukanda wa viwanda na uwekezaji.

Alisema kwasasa viwanda vilivyopo ni 200 ambavyo vipo vikubwa,vidogo na vya kati na mabavyo vimeanza kazi,vinavyoendelea na mchakato na vingine hatua za mwisho za ujenzi .

Akizungumzia masuala ya ulinzi na usalama ,aliwataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na kuacha kuamini wageni wanaoingia katika maeneo yao.

“Ukiona kuna mtu yupo kijijini ama kwenye mtaa wako humjui na unamtilia shaka basi toeni taarifa kwenye vyombo vya dola ili viweze kumfuatilia”

Hakusita kukemea migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu kwa kujeruhiwa ma kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa mhandisi Ndikilo,migogoro hiyo haina tija miongoni mwao na kusisitiza umoja,upendo na amani katika pande hizo mbili .

Alisema wamejipanga kuongea na mhimili husika ili kuuomba kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kutoa hukumu badala ya kupiga faini.

Mhandisi Ndikilo alisema wafugaji wakitozwa faini wamekuwa na kiburi na dharau kutokana na kuwa na uwezo wa kulipa hivyo kuanzia sasa wapigwe kifungo ili kukomesha jeuri yao.

Katika hatua nyingine amewataka wazazi na walezi kusomesha watoto wao wa kike na wakiume pasipo kuwabagua kwani elimu ni ufunguo wa maendeleo ya maisha yao ya baadae.

Nae katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji mkoani Pwani,Shangwe Twamala alisema ziara hiyo ililenga kutembelea maeneo yenye uzalishaji wa mazao ya kilimo cha biashara kama kwenye maghala ya korosho na viwanda vya matunda.

Pia kutembelea mashamba ya wakulima wa mihogo na kuhimiza kilimo kinachostahimili ukame ikiwa ni pamoja na mhogo,mtama,mikunde na viazi vitamu.

Twamala alisema wananchi wanapaswa kujiwekea utaratibu wa kucheza na misimu ya mvua kwa kulima mazao yanayotakiwa ili kukabiliana na uhaba wa njaa.

Katika ziara hiyo mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Ndikilo alitembelea maeneo ya Mji wa Rufiji,Mkuranga,Kibiti,Bagamoyo,Chalinze,Kisarawe na Kibaha.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania