CURRENT NEWS

Tuesday, May 2, 2017

RC NDIKILO -WAFANYAKAZI WAJITUME KWENDA NA KASI YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

Tokeo la picha la evarist ndikilo
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani 

MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, amewaasa wafanyakazi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajitume ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda inafanikiwa. 

Alisema wakati serikali inatekeleza kwa vitendo ujenzi wa viwanda katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo haina budi kila mmoja akachapakazi kwa bidii. 

Alitoa rai hiyo ,wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa serikali na sekta binafsi kwenye viwanja vya shule ya msingi Majengo wilayani Bagamoyo. 

Mhandisi Ndikilo, alieleza mtumishi wa kila sekta mkoani humo anapaswa kuwajibika kikamilifu ili kuongeza maendeleo. 

Alisema kuhusu maslahi ya wafanyakazi, serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri yatakayosababisha watumishi wa umma na sekta binafsi kuwa na morali ya kujituma.  

Aidha mhandisi Ndikilo alisema, wakati serikali ikitekeleza azma ya ujenzi wa viwanda jamii iendeleze watoto wao kielimu kwa lengo la kupata ajira baadae.

Nae Katibu wa TUICO mkoani hapo, Kassim Matewele, alieleza pamoja na jitihada za serikali za kutatua kero za wafanyakazi lakini bado wa sekta binafsi wanakabiliwa na tatizo la kufanyakazi bila mikataba. 

Alisema jambo hilo linawanyima haki zao kama wafanyakazi na kushindwa kuwekewa akiba zao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. 

Kwa mujibu wa Matewele, hali hiyo pia inasababisha serikali kupoteza kodi ambayo ingeweza kuingizwa kupitia pato la wafanyakazi hao. 

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania