CURRENT NEWS

Monday, May 22, 2017

VYAMA VYA SIASA VYATAKIWA KUINGILIA KATI MAUAJI YA KIBITI


Na Mwandishi Wetu,Pwani
BAADHI ya wananchi wilayani Kibiti ,mkoani Pwani ,wamewataka viongozi wa vyama vya siasa vikubwa wilayani humo, Chama cha Mapinduzi (CCM) na CUF ,kukaa meza moja kuangalia namna ya kukemea vitendo vya mauaji vinavyoendelea kwenye ukanda huo.
Aidha wamesema kwa umoja wao kutawezesha kushirikiana na serikali kumaliza janga hilo.
Pia wameiomba serikali kupeleka askari wa JWTZ kutanda katika wilaya za Rufiji na Kibiti hadi maeneo ya vijijini ili kudhibiti vitendo hivyo vinavyomaliza watu wasio na hatia .
Hata hivyo ,wameitaka serikali kuwadhibiti wahamiaji haramu wanaoingia kwenye njia za panya zilizopo Pwani kwani yawezekana baadhi yao wanaweza kuhusika katika matukio hayo.
Hadija Issa ,Hamis Kidongezo na Seif Mohammed waliyasema hayo,baada ya waziri wa mambo ya ndani ,Mwigulu Nchemba na mkuu wa Mkoa huo mhandisi Evarist Ndikilo ,kwenda kuzungumza na wananchi katika maeneo hayo.
Walieleza ,CCM na CUF taifa,mkoa na wilaya wanapaswa kutupia macho suala hilo kwa upana ili kubaini chanzo halisi kinachosababisha wauawe.
Hadija alisema ,inashangaza vifo vinavyoendelea kutokea wanakufa sana viongozi wa chama fulani lakini wapo viongozi wa vyama vingine wamenyamaza kama vile hakuna kinachoendelea.
Alisema serikali na askari polisi wanafanyakazi nzuri lakini inabidi kujulikane kina cha tatizo.
Hadija alieleza ,ugaidi unaweza ukawepo lakini anadhani pia kina chembe ya masuala ya kisiasa ."Yaani sidhani km vyama vingine vingepigwa kiasi hicho ingekuwaje "
"Naona kuna haja ya vyama vyote vikaguswa na hili ,maana hii agenda lisingekuwepo bunge ina maana viongozi wa vya vingine vinavyokuwa na sauti kubwa ya kutetea mengi wasingeongeaa"
"Tunaomba wanasiasa ,na wanaharakati wapige kelele kwa hili kama ilivyo katika mambo mengine ya kijamii wanavyofanya" alisema Hadija .
Hamis alielezea kwamba ,bado wananchi ambao ni wanachama na viongozi wa CCM, wanashindwa kuvaa sare za chama na kuogopa kuitana majina ya vyeo vyao.
Seif, alisema baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wanashindwa kwenda ofisini kutekeleza majukumu yao.
Alisema wanaishi kwa sintofahamu na imani inawatoweka.
Seif alifafanua, watu wanakiogopa chama kwasasa na kukimbia miji ,ofisi na kushindwa kuchukua fomu kugombea nafasi za ndani 
Anaeleza miaka ya nyuma watu walikuwa wakigombea nafasi mbalimbali za uongozi lakini kwa sasa wanakwepa na kuhofia uhai wao.
Seif aliiomba serikali kuwadhibiti wahamiaji haramu kwa kuwarudisha makwao badala ya kuachiwa kwani yawezekana wakaleta athari kubwa ndani ya Mkoa na taifa kijumla .
Katibu wa CCM Kibiti, Zena Mgaya, alisema ,serikali inaendelea na hatua za kiulinzi na usalama kwa wananchi na kuhusu ombi la wananchi wanalibeba .
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo, aliwaomba wananchi washirikiane na serikali kuwafichua wahalifu .
Ndikilo ,alieleza wauaji ama wahalifu wapo ndani ya jamii hivyo endapo wananchi wataamua kuwataja watu hao itawasaidia kuwakamata kirahisi.
Mkuu huyo wa Mkoa ,aliwataka kuwasema pia wageni kwenye maeneo yao kwani wageni wengine sio watu wema.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga alibainisha kwamba,wanaendelea kupambana kufuatia matukio hayo na kuimarisha ulinzi .
Ni matukio takriban 21 ya mauaji ya viongozi mbalimbali wa chama, wenyeviti wa vijiji /vitongoji na askari polisi ambayo yanadaiwa kujitokeza wilayani Rufiji ,Mkuranga na Kibiti.
Katika matukio hayo ni pamoja la March 28 ambapo mwenyekiti wa (CCM) tawi la  Mparange na mjumbe wa serikali ya kijiji cha Ikwiriri Kaskazini ,Michael Lukanda,aliuawa kwa kupigwa risasi ya kichwani .
Jingine ni march 12,mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo Hemed Njiwa aliuawa kwa kupigwa risasi.
Jan 19,mjumbe wa serikali ya kijiji cha Nyambunda ,Oswald Mrope, aliuawa kwa kupigwa risasi.
March 1,mwenyekiti wa kijiji cha Nyambunda Said Mbwana aliuawa.
Feb 24,watu watatu akiwemo afisa upelelezi wa polisi wilaya ya Kibiti Peter Kubezya aliuawa kwa risasi.
April 13 mwaka huu,yalitokea mauaji ya askari polisi nane waliouawa kwa kupigwa risasi na wahalifu waliokuwa na silaha za moto .
Octoba 24,2016 afisa mtendaji wa kijiji cha Nyambunda Ally Milandu alipigwa risasi na kufa.
Novemba 6,2016 ,mwenyekiti wa kitongoji cha Nyang'unda kijiji cha Nyambunda Mohammed Thabiti alipigwa risasi akielekea kwake.
Matukio mengine ni sanjali na May 17 ,mwenyekiti wa CCM tawi la Njianne ,kijiji cha Muyuyu ,ambae pia ni mjumbe wa kamati ya siasa kata ya Mtunda ,Iddi Kilungi ,aliuawa kwa kupigwa risasi.
May 13 mwaka huu,katibu wa CCM kata ya Bungu ,wilayani humo,Halife Mtulia ,kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. 
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania