CURRENT NEWS

Thursday, May 4, 2017

WAZIRI MWAKYEMBE AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA SHIRIKISHO LA SANAA ZA UFUNDI

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb), amekutana na Bw.  Adrian Nyangamalle - Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi  (TAFCA)  leo tarehe 4 Mei, 2017,  Dodoma.

 Bw. Adrian aliambatana na Bi. Francisca Shirima  - Makamu Rais wa TAFCA,  Bw. Godfrey Ndimbo - Katibu Mkuu wa TAFCA, Bw. Robert Mwampemba - Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Bi.Teddy Qirtu na Bw. Maclean Geofrey kutoka kampuni ya Data Vision. 

Uongozi wa TAFCA ulielezea kuhusu mradi wake mpya wa kuwasajili kielektroniki wanachama wake zaidi ya milioni 4 nchini kwenye mfumo wa kanzidata ili kuwatambua rasmi na kuwawezesha kutumia fursa mbalimbali. Katika mradi huo, TAFCA wanashirikiana na kampuni ya Data Vision.

 Kwa upande wake Mhe. Mwakyembe alimshukuru Bw. Adrian kwa kumtembelea na kumuahidi ushirikiano katika  masuala ya sanaa yanayosimamiwa na TAFCA. Mhe. Mwakyembe pia aliwataka TAFCA kusimamia haki za wanachama wake kwa kulinda maeneo yao ya kazi hususan eneo la kuchongea vinyago la mwenge, Dar es Salaam. 

"Nimefurahi kusikia kwamba mmeamua sasa kutengeneza mfumo wa kielektroniki wa kuwatambua na kuwasajili wanachama wenu, nawachagiza muukamilishe mfumo huu mapema kwa kuwa una faida lukuki kwa wanachama", alisisitiza Mhe. Mwakyembe. 

Aidha, Mhe. Mwakyembe aliwahakikishia TAFCA kwamba atawasiliana na COSOTA ili kuweka mfumo bora wa kulinda haki za kazi za sanaa nchini. Aidha, Mhe. Mwakyembe alitoa rai kwa uongozi wa TAFCA kujipanga na mabadiliko ya kasi kwenye biashara za sanaa yanayotokea ulimwenguni kwa sasa ili kulinda maslahi ya wanachama na nchi kwa ujumla.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania