CURRENT NEWS

Sunday, June 25, 2017

DC MTATURU AWAASA WAISLAMU KUENDELEZA TABIA NJEMA


Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akitoa neno la shukrani kwa waliohudhuria futari aliyoiandaa

 Kadhi wa mkoa sheikh Ramadhan Kaoja  akitoa neno la shukrani baada ya futari.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akimshukuru mwenyekiti wa CCM wilaya kwa kuhudhuria futari.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akimshukuru kadhi wa mkoa sheikh Ramadhan Kaoja baada ya kutoa neno la shukran.


 Baadhi ya wananchi waliohudhuria futari hiyo wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Miraji Mtaturu hayupo pichani

Viongozi waliohudhuria  wakiitikia dua baada ya kupata  futari kuanzia kushoto ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Ally  Mwanga,Sheikh wa wilaya hiyo  Abdi Seleman,mkuu wa wilaya hiyo Miraji Mtaturu katikati,mwenyekiti wa CCM wilaya Hassan Tati na kadhi Mkoa  wa Singida  Sheikh Ramadhan Kaoja.
.................................................................................................................

MKUU wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida  Miraji Mtaturu amewafuturisha waislamu wa wilaya hiyo huku akiwaasa kuendeleza tabia njema kwa mujibu wa kitabu cha Mwenyezi Mungu Quran hata baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan kumalizika.

Akizungumza na waislamu hao baada ya kupata futuru wilayani humo Mtaturu alisema katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan watu wametenda mema yanayopaswa kuendeleza hata baada ya mwezi huo.

"Wakati tupo kwenye mfungo huu tupo kwenye darasa la tabia njema hivyo nawashauri hata baada ya mfungo huu tuyaendeleze,"alisema Mtaturu.

Alisema serikali inafarijika pale inapoona wananchi wake wakifuata imani za dini zao na hivyo kuwa raia wema na nchi kuendelea kuwa na amani.

"Tunamaliza kukamilisha moja ya nguzo  tano za uislamu panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu,nawaombeni isiwe mwisho wa kufanya mema bali iwe ni mwendelezo katika siku zetu zote za maisha yetu,"alisisitiza Mtaturu.

Mtaturu aliwatakia maandalizi mema ya sikukuu ya Eid El Fitri huku akiwaasa kusherehekea kwa amani,utulivu na upendo na kukumbuka kutoa Zaka kwa watu wasio na uwezo.

Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kumuombea Rais Dokta John Magufuli kutokana na kazi kubwa anayoifanya katika  kuendeleza  dhamira yake ya kulinda rasilimali za nchi ili ziwanufaishe watanzania wote hasa wale wanyonge.

Kwa upande wake, Sheikh wa wilaya hiyo Abdi Seleman akitoa neno la shukrani alimshukuru mkuu wa wilaya huyo kwa kuwafuturisha na kusema hiyo ni mara ya kwanza toka wilaya hiyo ianzishwe kwa mkuu wa wilaya kuwaalika futari.

"Kwa sadaka yako hii kwetu tunamuomba  Mwenyezi Mungu akulipe kila la kheri,na inshallah huu usiwe mwisho bali uwe mwanzo wa kufanya hivi,"alisema Sheikh Seleman.

Naye, Kadhi wa mkoa wa Singida Ramadhan Kaoja alimshukuru  mkuu wa wilaya huyo na kusema hiyo ni dalili za kiongozi bora kwa kuwa karibu na jamii lakini pia ni sehemu ya kukamilisha imani yake ambapo kwa mwezi huu wa Ramadhan kwa kufuturisha anapata thawabu nyingi sana.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania