CURRENT NEWS

Saturday, June 17, 2017

DC MTATURU AWAOMBA WATANZANIA KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI KUOKOA RASILIMALI ZA NCHI

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu (katikati)akisisitiza jambo kwa mmiliki wa mgodi wa Mzacky na wenzake uliopo kijiji cha Mulumbi alipofanya ziara na kuzungumza na wachimbaji wadogo.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akimuhoji mmoja wa wachimbaji wadogo wa mgodi wa Elizabeth Shango kuhusu namna wanavyochonga 
miamba ya madini

Moja ya Shimo linaloandaliwa kwa ajili ya kuanza uchimbaji wa madini kwenye mgodi wa Magoma- Sambaru.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akikagua mitambo ya uchenjuaji wa dhahabu katika mgodi wa Magoma uliopo kijiji cha Sambaru.
 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akiwa pamoja na msafara wake walipotembelea  migodi na hapo ni maeneo ya mgodi wa Sambaru.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akikagua mitambo ya uchenjuaji wa dhahabu katika mgodi wa Magoma uliopo kijiji cha Sambaru. 

................................................................................................................................................................
MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu amewaomba watanzania kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli katika jitihada anazoendelea nazo za kupigania rasilimali za Taifa.

Aidha ametoa onyo kwa wabunge,madiwani na wenyeviti wa vijiji wa wilaya hiyo wanaotumia majukwaa ya siasa kubeza na kutaka kukwamisha juhudi hizo za rais na kusema kamwe hawatawavumilia watu hao.

Mtaturu ametoa ombi hilo wilayani humo alipowatembelea wachimbaji wadogo na kuzungumza nao ikiwa ni njia mojawapo ya kuunga mkono juhudi hizo za rais Magufuli katika sekta ya madini ambapo amesema rais anafanya kazi kubwa na nzuri kwa maslahi ya watanzania hivyo ni jambo jema kuunga mkono nia njema aliyonayo.

“Mheshimiwa Rais anawapenda sana na anawaunga mkono katika shughuli zenu na serikali yake inaahidi kuendelea kuwapa ruzuku za mitaji ya kuwasaidia kuboresha uchimbaji wenu ili uwe na tija,jambo jema kwetu ni kumuunga mkono,”alisema Mtaturu.

Katika mazungumzo hayo aliwaasa wachimbaji kuwa na ushirikiano na jamii inayowazunguka,kuchangia huduma za kijamii na kujenga utaratibu wa kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa sheria huku akimpongeza mchimbaji Yusuph Mwandami aliyewekeza mashine ya kuchomea carbon yenye dhahabu hatua ambayo amesema itapunguza gharama za kusafiri kwenda Mwanza.

Mtaturu aliishauri wizara ya nishati na madini kuangalia upya leseni waliyotoa kwa kampuni ya Shanta Gold Mine ambayo toka mwaka 2006 wapewe leseni hiyo mpaka sasa hawajaanza uchimbaji tofauti na wachimbaji wadogo ambao wana miezi mitatu tangu wapewe leseni lakini tayari wameshaanza uzalishaji na hivyo kushauri kufuta leseni kwa kampuni za aina hiyo ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wengine wenye nia njema.

“Nawaalika wawekezaji wenye nia ya kufanya uchimbaji mje Ikungi kwa sababu dhahabu ya hapa ni bora kitaalam  purit yake ni asilimia 91- 96 lakini pia nawakumbusha wachimbaji mlioanza kuzalisha mlipe mrahaba na tozo ya huduma ya halmashauri na katika hili mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hakikisha hadi kufikia julai mosi mwaka huu wote wanaodaiwa wawe wamelipa,”alisisitiza Mtaturu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Sambaru Hassan Maganga alimpongeza rais Magufuli kwa hatua anazochukua kwak uwa zitasaidia kuiwezesha nchi kupata mapato yatakayopelekea kuimarisha huduma kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo meneja wa mgodi wa Elizabeth Shango,ndugu Emmanuel Mwanga aliishukuru serikali kwa kuwapa ruzuku iliyowasaidia kununua vifaa mbalimbali na kutoa ombi la kuendelea kupata ruzuku ili wanunulie winchi ya kutolea mizigo kwenye mashimo huku akiweka bayana changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme waliyonayo inayopelekea kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.

Akijibu changamoto hiyo, Mtaturu 
aliwahakikishia kuwa kupitia mpango kabambe wa upelekaji umeme vijijini(REA III) itafikisha umeme vijiji vitatu vya kata ya Mang'onyi ambavyo ni Mang'onyi,Mwau na Mulumbi.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania