CURRENT NEWS

Sunday, June 11, 2017

KIWANDA CHA SAYONA CHAIPIGA TAFU CHALIWASA PAMPU 9 ZA SH.MIL.100

 Afisa mahusiano wa kampuni Mama ya MMI Steel na kiwanda cha Sayona kilichopo Mboga, Chalinze Mkoani Pwani,Abubakar Mlawa ,akizungumzia namna wanavyoshirikiana na jamii
MBUNGE wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ,wa kwanza kushoto akiwa katika kiwanda cha Sayona kilichopo Mboga jimboni Chalinze, kujionea hali ya ujenzi unavyoendelea(picha na Mwamvua Mwinyi )


Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MWEKEZAJI wa kiwanda cha kusindika matunda (SAYONA)kilichopo ,Mboga-mkoani Pwani,Subhash Patel ,ametoa mitambo Tisa ya kusogeza maji kwa mamlaka ya maji Chalinze-CHALIWASA ,iliyogharimu sh.mil.100 .
Mitambo hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za maji baada ya kuona changamoto za mitambo ya awali imefikia pabaya kutokana na kufungwa miaka mingi iliyopita .
Akizungumzia kuhusiana na mchango huo,kiwandani hapo,afisa mahusiano wa kampuni mama ya MMI steel na Sayona ,Abubakar Mlawa alisema ,wanaiunga mkono serikali kwa jitihada zake.
Alielezea kwamba ,mitambo hiyo imenunuliwa kutoka China ,na kinachosubiriwa sasa ni mamlaka ya maji kupitia na kuingia mkataba ili ifungwe .
Mlawa alisema ,utekelezaji ukishafanyika mapema itawezesha huduma ya maji kupatikana kwa wakazi wa Chalinze na maeneo mengine yanayohudumiwa na kituo cha WAMI -Chaliwasa .
Aidha alisema ,mitambo hiyo wameitoa kama mkopo nafuu ili kupisha serikali iendelee kujipanga utekelezaji mwingine na watalipana kwa malipo ya bill ya maji.
"Kampuni yetu ,ikiwemo Sayona tunashirikiana na jamii kusaidia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa madarasa ,kununua zima moto na kuchangia shughuli za maendeleo " alisema Mlawa .
Nae mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete ,alimpongeza mwekezaji huyo kwa moyo wake wa kujitoa.
Alisema ,ujenzi wa viwanda unahitaji maji na ili kuvutia wawekezaji Chalinze na mkoa kijumla ni lazima maji yawepo ya uhakika .
Ridhiwani alibainisha kwamba ,wapo wawekezaji wawili akiwemo Sayona ambao wamejitokeza utayari wa kufuata taratibu za serikali kusaidia tatizo la maji .
"Malengo makubwa ni Chalinze kuwa na maji ya uhakika inawezekana na sidhani kama lengo lao ni kujipendelea kupata maji ya peke yao " alifafanua Ridhiwani .
Mbunge huyo ,alisema ,endapo mitambo hiyo itafikia vigezo na ubora unaotakiwa na wizara husika kisha kupitishwa itasaidia Mji wa Chalinze na vijiji vingi kupata maji ya uhakika .
Ridhiwani ,alisema juhudi za serikali za kupambana na kumtua ndoo mama kichwani kwa kushirikiana na wadau na wawekezaji itafanikiwa kwa umoja wao.
Meneja wa mamlaka ya maji Chalinze-CHALIWASA ,Christer Mchomba ,alisema mwekezaji Sayona ameonekana kuwa shapu yangu kutoa ahadi yake na wanamshukuru .
Alisema alijitokeza kuandika barua wizarani kuomba kuchangia CHALIWASA ili kuboresha huduma za maji .
Christer alisema ,hatua iliyopo sasa ni kupitiwa kwa pampu hizo kwa kuzikagua kiufundi na ubora,kuona kama zinakidhi mahitaji .
Wakati huo huo akielezea kuhusiana na hali ya mitambo ilivyo ,alisema mitambo ya WAMI zaidi ni ya Kichina ambayo ni ya zamani mengine hivyo inatakiwa kuiondoa.
Alisema kutokana na usanifu uliokuwepo kwa maji ya mto WAMI haiwezekani kuendesha mitambo ya Kichina kwa maji ya tope yaliyopo .
"Hali ya huduma ya maji Chalinze ilikuwa sio nzuri ,lakini endapo nguvu itaunganishwa kuanzia Mvomero ,Chalinze,Gairo kupambana na watu wanaofanya shughuli za binadamu karibu na vidaka maji vya mto tatizo la maji litabaki historia "
"Wakati tukisubiri mradi ukamilike basi tuendelee kubadilisha pampu ziwepo za dharura ili kukabiliana na hali iliyopo " alisema Christer .
Christer alisema ,alishatafutwa pia mzabuni na kupeleka pampu nne ambazo mbili zitakarabati kivuko cha maji WAMI ,na kimoja kwenye Kituo cha Mandela .
Alisema kuwa ,vituo hivyo ni vikubwa ambapo pampu zinavuta maji kutoka shimoni kupandisha kuvuta juu na kama pampu zikishindwa kuvuta maji ".Yanakuwa hayafiki kusambaa kwenda kwenye maeneo mbalimbali .
Kiwango cha tope katika mto Wami nyakati za mvua nyingi tope huongezeka na kufikia NTU 15,000.
Licha ya changamoto zote hizo ,serikali iliendelea kuchukua hatua za kuondoa tatizo la maji tangu mwaka 2001 kwa kutekeleza mradi wa maji chalinze kwa awamu mbalimbali.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania