CURRENT NEWS

Thursday, June 1, 2017

MWENGE WA UHURU WAINGIA PWANI NA KUANZA MBIO ZAKE MAFIA


Na Mwamvua Mwinyi ,Pwani
MWENGE wa Uhuru umeanza mbio zake mkoani Pwani ambapo unatarajia kutembea miradi 81 yenye thamani ya sh.bil 225.1.

Akipokea mwenge huo kutoka mkoa wa Dar es Salaam,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo, alisema kati ya miradi hiyo ,27 itawekewa mawe ya msingi, na miradi 27 itazinduliwa na minne itafunguliwa na miradi 25 itakaguliwa.

Miradi hiyo yote imechangiwa kwa pamoja na wananchi, serikali kuu, Halmashauri na wahisani wa ndani na nje .

Mhandisi Ndikilo alisema  mkoa huo unatekeleza kwa vitendo ujumbe wa mwenge “Shiriki kukuza uchumi wa Viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu” ambapo kwa sasa una viwanda 264.

“Kati ya hivyo viwanda vikubwa ni 84 na vidogo 186 na kila Halmashauri imetenga maeneo kwa ajaili ya uwekezaji na kuna fursa nyingi sana za uwekezaji kwenye mkoa wetu na tumeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema mkoa huo una maeneo maalumu ya kibiashara Mkiu wilaya ya Mkuranga na Bagamoyo kwa ajili ya fursa za uwekezaji wa aina mbalimbali vikiwemo viwanda.

“Tunawakarisha wawekezaji toka nje kwani kuna miundombinu mizuri imewekwa kwa ajili ya uwekezaji ili kuwa kivutio na mazingira yameboreshwa ili kufanikisha kauli mbiu hiyo,” alisema Ndikilo. 

Alieleza mbali ya kuhimiza uwekezaji wa viwanda pia wanapambana na maradhi ya ukimwi na malaria dawa za kulevya na rushwa.

Mwenge huo umeanza mbio zake wilayani Mafia june 1 na june 2,utakuwa wilayani Rufiji.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania