CURRENT NEWS

Friday, June 9, 2017

RAIS MAGUFULI APONGEZWA KWA UZALENDO

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi  Hassan Tati akifungua kikao maalum cha halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Ikungi


 Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi  Hassan Tati akiongoza kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya kulia kwake ni mkuu wa wilaya hiyo Miraji Mtaturu,katibu wa CCM wilaya  Elieza Philipo na kushoto kwake mwenyekiti wa halmashauri ambaye ni diwani wa kata ya Irisya  Ally  Mwanga.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu  akitoa salaam za serikali kwenye kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya.


Wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Ikungi  wakiwa kwenye  kikao maalum.
....................................................................................
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)wilaya ya Ikungi mkoani Singida imempongeza Rais Dk.John Magufuli kwa hatua mbalimbali anazozichukua za kizalendo toka aaminiwe na watanzania na kupewa ridhaa ya kuongoza dola katika serikali ya awamu ya tano.

Kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka halmashauri kuu hiyo imeahidi kuendelea kumuunga mkono katika mambo mbalimbali anayoyafanya ikiwemo vita ya wabadhirifu wa rasilimali za Taifa ikiwemo madini.

Akitoa pongezi hizo ndani ya kikao hicho mwenyekiti wa CCM wilaya Hassan Tati amesema rais Magufuli amejipambanua wazi dhamira yake aliyonayo ya kuiona Tanzania mpya yenye uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kuondoa rushwa miongoni mwa jamii ambayo ilikuwa kikwazo kikubwa kwenye mfumo wa kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Sisi halmashauri kuu ya wilaya tunatoa pongezi zetu za dhati kwa mheshimiwa rais ambaye anatimiza majukumu yake kwa weledi,anatimiza yale aliyoyaahidi,pamoja na pongezi hizo tunamshukuru kwa kutuletea mkuu wa wilaya mchapakazi Miraji Mtaturu,”alisema Tati.

Alisema tangu mkuu huyo wa wilaya afike amefanya kazi kubwa ya kuhamasisha maendeleo kwa wananchi na matunda yameanza kuonekana na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwake ili malengo ya kuifanya Ikungi yenye maendeleo yaweze kufanikiwa.

Aidha walimpongeza mbunge wa Singida Magharibi Elibariki Kingu kwa juhudi zake anazozionyesha katika kuwahudumia wananchi waliomchagua kupitia Ilani ya CCM aliyoinadi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 katika kikao hicho Mtaturu alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ambapo mpaka sasa utekelezaji wa utoaji wa elimu bila ya malipo umefanikiwa ambapo toka Januari mwaka jana wilaya hupokea shilingi milioni 39.9 kwa mwezi ikiwa ni ruzuku kwa ajili ya shule za sekondari na shilingi milioni 36 kwa elimu ya msingi.

Katika sekta ya afya alisema wilaya kwa kushirikiana na wadau wengine na wananchi  imedhamiria hadi kufikia mwaka 2018 zaidi ya asilimia 50 ya vijiji viwe na Zahanati ambapo wilaya hiyo ina jumla ya vijiji 101 huku kukiwa na zahanati 37 kati ya hizo 34 za serikali na 3 binafsi lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kupata huduma ya afya karibu kama ilani ya uchaguzi inavyoelekeza.

"Upande wa sekta ya nishati kupitia mpango kabambe wa usambazaji umeme vijijini(REA III) vijiji vipatavyo 44 vitapata umeme na kwa sasa mkandarasi yupo kazini,nawaomba wananchi wafanye maandalizi ya kupokea huduma hiyo ambayo itasaidia kuinua uchumi wa wananchi katika kuelekea nchi ya kipato cha kati,"alisema Mtaturu.

Alitumia nafasi hiyo kuhamasisha kilimo na kueleza kuwa wilaya kwa kushirikiana na bodi ya korosho wamedhamiria kupanda mikorosho kutokana na eneo hilo kuonekana linafaa kwa kilimo hicho kwa mujibu wa utafiti ambapo ili kuhakikisha hilo linafanikiwa wamejipanga kugawa bure miche ya mikorosho kwa wananchi.
x
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania