CURRENT NEWS

Friday, June 9, 2017

WATATU WADAIWA KUFA KIBITI KWA KUPIGWA RISASI

Na Mwamvua Mwinyi ,Kibiti
Watu watatu wakazi wa kijiji cha Nyamisati, wilayani Kibiti wanadaiwa kufariki dunia kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia june 9 na watu wasiojulikana.
Ndani ya siku saba watu wanne wameshakufa kwa kupigwa risasi Kibiti na Rufiji ,mmoja amenusurika kifo kwa kupigwa risasi ya kichwa na mmoja ametekwa .
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema  miongoni kwa watu waliouwawa yupo mwenyekiti wa kitongoji  Moshi Machela.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao watu waliouuwawa ni Hamid Kidevu,Yahaya Makame na Moshi Machela.
Mkuu wa wilaya ya Kibiti Gulamuhusein Kifu alithibitisha kutokea kwa tukio hili June 8 mwaka huu .
Alisema kwamba amepokea taarifa ya kutokea kwa mauaji hayo na hivyo bado hana taarifa zaidi licha ya kumuagiza OCD  kwenda eneo la tukio kwa uchunguzi zaidi .
"Lakini jeshi na askari polisi  bado wapo  kazini wakiwasaka wahalifu hawa wanaoendelea kumaliza watu wasio na hatia ," alisema Kifu .
Mnamo june 7 majira ya saa 7,Nurdin Mohammed Kisinga ,alijeruhiwa baada ya kupigwa risasi ya kichwa ,na watu wasiojulikana huko kijiji cha Ngomboroni kata ya Umwe Kaskazini,Ikwiriri wilayani Rufiji.
Hata hivyo ,mkazi mwingine,Eric Mwarabu ambae alikuwa ni askari mgambo alifariki mara baada ya kupigwa risasi nyumbani kwake.
Pia maiti ya mwanaume ambae hajajulikana jina iliokotwa mchana june 7 huko kijiji cha Mtunda A,kitongoji cha Ngwaro,kata ya Mtunda wilaya ya Kibiti.
Katibu wa Chama Cha Mapinuzi CCM ,kata ya Mtunda ,Abdallah Mayonjo alieleza,maiti hiyo iliokotwa ikiwa imefungwa kamba mikononi na miguuni.
Mbali ya hayo ,mtu mwingine ameokotwa akiwa amefariki dunia kijiji cha Kipoka ,Ikwiriri wilayani Rufiji  huku ikiwa haina nguo.
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania