CURRENT NEWS

Tuesday, June 13, 2017

WATUMISHI 10,931 WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA WAPEWA MAFUNZO YA UHASIBU Mkuu wa Mifumo ya Mawasiliano PS3 bwana Desderi Wengaa akizungumza mafanikio yaliyopatikana kwa watumishi 10931 wa Halmashauri 93 ambazo zinatekeleza Mradi wa PS3 nchini.


Baadhi ya waratibu elimu kata na waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Lindi na halmashauri ya wilaya ya Lindi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura wakati alipoyafungua mafunzo hayo katika mkoa wa Lindi.


Baadhi ya waratibu elimu kata na waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Lindi na halmashauri ya wilaya ya Lindi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura wakati alipoyafungua mafunzo hayo katika mkoa wa Lindi 
Baadhi ya watoa mada ambao ni wahasibu kutoka Manispaa ya Lindi na halmashauri ya wilaya ya Lindi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura wakati alipoyafungua mafunzo hayo katika mkoa wa Lindi. 

 Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI bwana Lucas Mrema akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Lindi.

 Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura wakati akifungua mafunzo ya waratibu elimu kata na waganga wafawidhi kutoka Manispaa na halmashauri ya wilaya ya Lindi.


Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura akiwa katika picha ya pamoja na waratibu elimu kata na waganga wafawidhi kutoka Manispaa ya wilaya ya Lindi. 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura akiwa katika picha ya pamoja na waratibu elimu kata na waganga wafawidhi kutoka halmashauri ya wilaya ya Lindi.
....................................................................................................................................................
Na Mathew Kwembe, Lindi

Jumla ya watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa 10,931 kutoka Halmashauri 93 za Mikoa 13 inayotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) wamepewa mafunzo ya uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha katika awamu ya kwanza na ya pili ya mafunzo hayo yaliyofanyika katika mikoa hiyo.

Mkuu wa Mifumo ya Mawasiliano PS3 bwana Desderi Wengaa ameyasema hayo jana mjini Lindi kabla ya kumalizika kwa awamu ya pili ya mafunzo hayo ambayo yaliwahusisha waratibu wa elimu kata na waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka mikoa 13 iliyo chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).

Bwana Wengaa amefafanua kuwa katika awamu ya kwanza ya mafunzo ambayo yalitolewa kwa wakufunzi waliowafundisha watumishi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa, jumla ya wakufunzi 2883 walipewa mafunzo hayo kwenye mikoa hiyo.

Akizungumza kabla ya kuhitimishwa kwa awamu ya pili ya mafunzo hayo yanayoendelea katika mkoa wa Lindi bwana Wengaa amesema kuwa katika awamu ya pili ya mafunzo jumla ya watumishi a Mamlaka za Serikali za Mitaa 10,048 kutoka Mikoa 13 inayotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) walifaidika na mafunzo ya uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha.

Ameongeza kuwa mara baada ya Waratibu wa Elimu kata na Waganga wafawidhi wa vituo vya afya kupewa mafunzo ya aina hiyo, watumishi hao watapaswa kwenda kuwapa mafunzo kama hayo kwa wahasibu katika ngazi ya shule na Zahanati.

“Lengo ni kuufanya mfumo wetu unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS) uanze kutumika ifikapo julai mosi, 2017 kama Serikali ilivyokusudia,” alisema.

Alisema kuwa mfumo huo umeundwa kuweza kukidhi changamoto mbalimbali za miundombinu, ikiwemo umeme, na kutokuwa na upatikanaji wa mtandao kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma katika halmashauri mbalimbali na hivyo mfumo huo hautakuwa tu katika muundo wa kielektroniki, lakini pia kutakuwa na muundo wa kujaza kwenye vitabu.

“Mfumo wa kujaza katika vitabu na wenyewe umeboreshwa na kuwa rahisi kwa mtumiaji kujaza taarifa sahihi, na huu utatumika kwa vile vituo ambavyo changamoto ya upatikanaji wa miundombinu wezeshi katika matumizi ya kielektroniki,” alisema na kuongeza kuwa mara baada ya kujaza katika vitabu, takwimu hizo zitaingizwa katika mfumo kwenye ngazi ya halmashauri na vituo kupatiwa taarifa ya vituo vyao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha kuwa wanatumia fursa hiyo kujipatia ujuzi ambao watakwenda kuutumia ili kuwezesha malengo ya serikali kufikiwa.

Bwana Satura aliongeza kuwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hawana budi kujifunza kwa bidii mafunzo hayo ili waweze kuandaa taarifa sahihi na kufunga mahesabu yao vizuri.

“Bila kufanya hivyo halmashauri zitaendelea kupata hati chafu na huku watendaji ake wakiitwa mchwa,” alisema.

Mfumo huo wa FFARS unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI); Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na USAID.

Mikoa 13 inayotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ni Mtwara, Lindi, Dodoma, Iringa, Mbeya, Njombe na Morogoro. Mikoa mingine ni Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Kigoma, na Kagera.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania