CURRENT NEWS

Monday, July 10, 2017

DC MTATURU ASHIRIKI JUBILEE YA PADRI MIKINDO NA KUTIMIZA AHADI YA MIFUKO 30 YA SARUJI.

Wanafunzi wa shule ya seminari ya Dung'unyi  wakipokea kwa furaha mifuko ya saruji ikiwa ni ahadi ya mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu aliyowahi kuitoa ya kusaidia uendelezaji wa ujenzi wa mabweni shuleni hapo.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akiwa ameongozana  na Askofu Bernad Mapunda na Mwenyekiti wa CCM wilaya Hassan Tati katika sherehe hiyo  ya jubilee.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu katikati akiongea na padri Emmanuel Missanga Mikindo na mwenyekiti wa CCM wilaya Hassan Tati katika tafrija ya jubilee.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akijadiliana jambo na Padre Emmanuel Missanga Mikindo wakati wa sherehe ya Jubilee
............................................................................
MKUU wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu ameshiriki Jubilee ya miaka 25 ya Padri Emmanuel Misanga Mikindo wa Kanisa  Katoliki Parokia ya Mitundu wilayani Manyoni mkoani Singida.

Akiwa katika ibada hiyo maalum pamoja na mambo mengine  Mtaturu alitimiza ahadi yake aliyoiwahi kuitoa ya kuchangia mifuko thelathini(30)ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya shule ya seminari ya Dung’unyi inayomilikiwa na kanisa hilo wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi.

Akizungumza katika ibada hiyo maalum iliyofanyika Parokia ya Dung'unyi wilayani Ikungi na kuhudhuriwa na mapadri na masista kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Singida mkuu huyo alimpongeza Padri Mikindo kwa kufikisha miaka 25 ya utume wake katika kanisa na kuwaomba waumini kuendelea kumuombea.

"Nilipongeze kanisa kwa kazi nzuri ya kuwaandaa waumini kiroho na hivyo kuwafanya kuwa raia wema,lakini pia kwa  kuendelea kusaidiana na serikali katika kutoa huduma za kijamii kama vile elimu,afya na huduma nyingine na naahidi kuendeleza ushirikiano huo katika kutatua changamoto zinazojitokeza kwa kuwa serikali  ya awamu ya tano imejipambanua  kuhakikisha huduma za kijamii zinaboreshwa,"alisema Mtaturu.

“Nilipokuwa kwenye ziara yangu shuleni hapo miezi miwili iliyopita nilikuta kuna ujenzi wa mabweni mawili na jiko,na niliahidi kuongezea nguvu na nafurahi kusema ahadi hiyo nimeitimiza ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi mnazozifanya katika kuwalea vijana wetu kimaadili na kitaaluma,”alisema Mtaturu.
Alieleza mikakati ya kuinua kiwango cha elimu wilaya humo ambapo wameanzisha mfuko wa elimu ambao dhamira yake kubwa ni kutatua changamoto za utoaji wa elimu katika shule za msingi na sekondari na kuliomba kanisa kushirikiana na serikali kuutunisha mfuko huo ili hatimae wazitatue changamoto hizo kwa pamoja.
"Upande wa uchumi wa wananchi kama  wilaya tumekuja na mkakati wa kupanda zao la korosho ambalo litakuwa mkombozi wa wananchi  kiuchumi  na katika utekelezaji huo wilaya tumejipanga kutoa miche bure na serikali kupitia wizara kilimo itatoa dawa ya sulpher bure kwa ajili ya upuliziaji na kuua wadudu waharibufu wa mikorosho,"alisema Mtaturu.
Alisema tayari wameanza  mazungumzo na wawekezaji ili kujenga kiwanda cha ubanguaji korosho wilayani Ikungi ili kuongeza mnyororo wa  thamani wa zao la korosho lakini pia ni hatua mojawapo ya kutekeleza agizo la  Rais mheshimiwa John Magufuli la kuwa na Tanzania ya viwanda.

Akitoa shukrani baada ya kupokea msaada huo wa saruji Baba Askofu Bernad Mapunda alimshukuru mkuu wa wilaya aliyeongozana na mwenyekiti wa CCM Wilaya  Hasan Tati kuja kushiriki tukio muhimu la Jubilee ya Padre  Mikindo na kusema ameonyesha
uaminifu wake wa kukamilisha ahadi aliyowahi kuitoa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo wa mabweni ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

“Ulipokuja kwenye ziara yako nilikuambia kuwa wewe ni mkuu wa wilaya wa kwanza katika kipindi cha miaka saba kufika katika shule ile,nashukuru Mungu amekubariki umetimiza ahadi yako,”alisema askofu Mapunda.

Shule hiyo ya Dung’unyi ilianzishwa mwaka 1996 ikiwa ni ya kidato cha kwanza hadi cha sita kwa michepuo ya Sanaa,biashara na sayansi ikiwa inapokea wanafunzi kutoka ndani na nje ya mkoa wa Singida.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania