CURRENT NEWS

Sunday, July 2, 2017

DC MWANGA -WAJASIRIAMALI KIMBILIENI KUDAKA FURSA ZA VIWANDA BAGAMOYO

Na Mwamvua Mwinyi ,Chalinze 
MKUU wa wilaya ya Bagamoyo ,mkoani Pwani ,alhaj Majid Mwanga ,ametoa rai kwa wanawake wajasiriamali kutumia kazi za mikono yao kuzalisha kwa wingi ili kunufaika na viwanda wilayani humo .
Aidha amewataka kutumia mikopo wanayopatiwa na halmashauri kwa manufaa ya kuzalisha badala ya kufanyia ufahari mitaani .
Kwa mujibu wa alhaj Mwanga ,mwanamke ni mipango ,mbunifu ,na mdakaji fursa .
Aliyasema hayo ,wakati wa uzinduzi wa jukwaa la uwezeshaji Chalinze ,lililoambatana na uchaguzi wa viongozi watakaoongoza kwa mwaka mmoja.
Alieleza ,biashara ni ushindani hivyo wanawake wakimbizane na fursa ya viwanda mbalimbali ikiwemo vya kusindika matunda ili kuondokana na umaskini .
Alhaj Mwanga ,aliwataka wawe wabunifu wa kutengeneza vitu vyenye ubora na kujitangaza pasipo kufanyabiashara kizamani .
"Tumieni mitandao ,boresheni bidhaa zenu ,na jitangazeni bila uoga ili mpige hatua " alisisitiza .
Hata hivyo,mkuu huyo wa wilaya alisema ,halmashauri zinatoa mikopo ya vijana na wanawake lakini haiwezi kufikia kundi kubwa endapo vikundi vilivyokwisha pewa havirejeshi kwa wakati lengwa .
Alhaj Mwanga aliomba vikundi vinavyonufaika na mikopo hiyo ,vijenge tabia ya kurejesha mikopo hiyo .
Nae mbunge wa viti maalum mkoani Pwani ,Subira Mgalu, alikemea tabia ya ubinafsi na ,badala yake wathubutu kujenga umoja utakaoweza kuwezeshwa kirahisi .
Alisema  taasisi ya uwezeshaji chini ya serikali , inatoa udhamini kwa umoja wa vikundi,na kudhamini kukopa kwenye taasisi za kifedha ikiwemo Tanzania Posta Bank, bank ya Wanawake -TWB na NMB .
Subira aliwaasa wanawake kuacha kujitenga na kuwa wachoyo wa kupeana njia za mafanikio .
Alisema Chalinze ina vikundi vingi vya wanawake na vijana lakini vimekuwa nyuma kuchangamkia maendeleo.
" Inabidi mpate elimu ya kutosha ,ili mvuke hapo mlipo ,.Hata kujitokeza sio kama ilivyo mji wa Kibaha na kwingine,vikundi ni vichache ,bidhaa mlizoleta kujitangaza ni kama hamna "alisema Subira .
Afisa maendeleo ya jamii Chalinze ,Antony Nyange ,alisema wameshatumia mil .200  kuwezesha vikundi vya wanawake na vijana.
" Kati ya fedha hizo mil.100 vimekopeshwa vikundi vya akinamama 35 na vikundi 34 vya vijana vimekopeshwa mil.100" alisema Nyange .
Nyange alielezea kwamba ,lengo la halmashauri ya Chalinze kwa mwaka ujao wa fedha ni kutenga mil .300 ili kuwesesha makundi hayo .
Katika uzinduzi wa jukwaa hilo ,kulifanyika uchaguzi ambapo Nyange ,alimtangaza Diana Mlaki kuwa mwenyekiti na Aisha Kombo ni Katibu kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao .
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania