CURRENT NEWS

Monday, July 17, 2017

HALMASHAURI YA CHALINZE -YAANZA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA ZILIZOHARIBIKA WAKATI WA MVUA

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
HALMASHAURI ya Chalinze ,wilayani Bagamoyo,imeanza kuboresha miundombinu ya barabara zilizoharibika vibaya wakati wa mvua kupitia fedha kutoka kwa wakala wa barabara (TANROADS)mkoani Pwani.
Aidha halmashauri imesema inajenga vyumba vya madarasa 60 katika shule mbalimbali kwa kushirikiana na nguvu za wananchi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze ,Saidi Zikatimu ,alisema  kiasi cha sh .mil.140 tayari kimetengwa kwa ajili ya kujenga barabara kutoka Vigwaza -Buyuni-Kidogozero yenye km .9.4 ambayo mawasiliano yake yamekatika.

"Barabara hii imeharibika sana ,imekata mawasiliano ,kwahiyo tunashukuru mvua zimekatika na kilichobakia ni kukarabati na kuboresha maeneo korofi yote ili kurahisisha usafiri na kuwaondolea adha wananchi " alisisitiza Zikatimu .
Alisema katika awamu ya kwanza wametenga pia sh .mil.131.979.1 na kandarasi ameshapatikana ambae atatengeneza barabara ya Kikalo-Kwaikonje -Gongo hadi Matipwili .
Barabara nyingine zikatakazotumika kwenye fedha hiyo ni Mkange-Gongo,Kwaruhombo-Kwamduma na Kibaoni hadi Kifureta .
Zikatimu alibainisha barabara za Lugoba -Talawanda ,Magurumatari-Talawanda ,Msata -Pongwe ,Magurumatari -Talawanda na Pingo-Kidogozero imetengwa mil.167 kwa ajili ya kuboresha barabara na makalavati .
Mwenyekiti huyo ,alitaja barabara nyingine iliyotengewa fedha ni Mboga-Diozile,Mdaula-Matuli na Lugoba- Moreto ambapo itatumika sh.mil.105 ./#.
Hata hivyo ,halmashauri hiyo imeshatumia mapato yake ya ndani kiasi cha sh.mil.150 kwa kujenga kalavati na barabara kutoka Kimange-Pongwe Kiona .
Katika kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa ,Zikatimu alibainisha kwamba ,wameshaanza kushirikiana na wananchi kujenga madarasa katika maeneo mbalimbali Chalinze .
Alisema hadi sasa vyumba hivyo vipo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi.
Alielezea kuwa ,kati ya vyumba hivyo Bwilingu wanajenga vyumba  16 kwa nguvu za wananchi lakini halmashauri imechangia mil.21 .
Magome wanajenga vyumba hivyo vitatu na halmashauri imewashika mkono kwa kuchangia mil.saba .
"Tumejipanga kuondoa uhaba wa madarasa ambao bado upo katika shule za msingi na sekondari" alieleza Zikatimu .
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania