CURRENT NEWS

Tuesday, July 25, 2017

JAFO AINYOOSHEA KIDOLE OFISI YA MGANGA MKUU MKOA WA KAGERA

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na Mbunge wa Karagwe Innocent Bashungwa wakiangalia baadhi ya miundombinu ya Zahanati ya Ihembe 2 yanayoanza kuharibika kutokana na kutotumika.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na viongozi mbalimbali katika ukaguzi wa Zahanati ya Ihembe 2 wilayani Karagwe.Nyumba ya Mganga wa Zahanati ya Ihembe 2 iliyotelekezwa licha ya kukamilika.
.............................................................................
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo ameendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ambapo akiwa katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera amekerwa na tabia ya baadhi watendaji kwa kutoguswa na matatizo ya wananchi na kuendekeza kukaa ofisini.

Akiwa wilayani humo leo, Jafo amesema watendaji hao wamekuwa wakikaa ofisini bila ya kufika maeneo ya wananchi na kubaini juhudi kubwa zinazofanywa na jamii na kwa upande wao kama wataalam waweze kufanya majukumu yao kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma.  

Naibu Waziri Jafo ameonyesha kukerwa na taarifa aliyoipata kwamba Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa wa Kagera imesababisha zahanati tatu zilizokamilika zimeshindwa kufunguliwa licha ya kukamilika kwa muda mrefu kutokana na mtazamo hasi wa Ofisi ya Mganga huyo.

“Zahanati hizo zilizo kamilika ni zahanati ya Ihembe 2, kategile,  na Lubale ambazo kwasasa miundombinu yake imetelekezwa bila kutumika licha ya wananchi kutumia nguvu kubwa kujenga miundombinu,”amesema Jafo

Naibu Waziri Jafo ameamua kulifanyia kazi jambo hilo ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma ya Afya kupitia zahanati hizo.

Hata hivyo Naibu Waziri Jafo amesema kwamba kama itabainika Afisa yeyote amefanya uzembe katika suala hilo Ofisi ya Rais Tamisemi itamchukulia hatua Kali kwa kukwamisha utoaji wa huduma ya afya.

Jafo anaendelea na ziara yake mkoani Kagera ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi  ya barabara, Afya, elimu, na Maji inayo simamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi).


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania