CURRENT NEWS

Thursday, July 20, 2017

MAKILAGI: WATAKAOTUMIA RUSHWA UCHAGUZI HUU UWT TUTAWATIA ADABU


NA BASHIR NKOROMO

Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) imeapa kuwa ya mfano katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wagombea wa nafasi mbalimbali katika Jumuia hiyo watakaobainika kutumia rushwa au kufanya vitendo vyovyote vinavyokiuka kanuni za Uchaguzi.
Kiapo hicho kimetolewa jana jijini Dar es Salaam, na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Amina Makilagi wakati akitangaza maazimio ya Kikao Cha Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UWT kilichofanyika juzi Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, jiijini.

"Tunashukuru kwamba baada ya Mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Dk. John Magufuli kuonyesha anapambana na rushwa kufa na kupona na kwa dhati kabisa, kila mtu amemuelewa na sisi UWT tunaahidi kumuunga mkono kwa kuhakikisha katika uchaguzi huu hatutakuwa na mzaha, yeyoyote atakayebainika kutumia rushwa hatutamuonea aibu hata awe nani", alisema Makilagi.

Alisema, uchaguzi kwa ngazi ya Matawi umefanyika kwa asilimia 95, ngazi ya Kata vikao vya uchujaji vinaendelea na kwa ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa uchaguzi unaendelea.

Makilagi alisema, kuanzia Julai 2 – 10, 2017 wanachama walipochukua fomu na kuzirejesha jumla ya wanachama 7,643 wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali ambapo kwa nafasiya Mwenyekiti wa UWT waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ni wanachama 34, nafasi ya Makamu Mwenyekiti wanachama 14, wajumbe wa NEC Bara 33, Baraza Kuu 73, Wawakilishi Vijana 15 na Wazazi 15, Upande wa Zanzibar wajumbe wa NEC ni 13 na Baraza Kuu ni 40.

Alisema hatua hiyo ya wanachama kujitokeza kwa idadi kubwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuliko chaguzi zilizopita kumethibitisha imani yao kubwa kwa Jumuiya na Chama Cha Mapinduzi.

"Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UWT imewapongeza wanachama wote waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea. Pia, inatoa mwito kwa wanachama wote kuendelea kuzingatia Kanuni za Uchaguzi na Maadili kwa kutotangaza nia, kutounda makundi na safu za kampeni pamoja na kujizuia kutoa na kupokea rushwa.

UWT inasisitiza kuwa, rushwa ni adui wa haki. Tutakuwa Jumuiya ya mfano, kwani hatutamvumilia yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa", alisema Makilagi. KUSOMA TAARIFA KAMILI YA KIKAO CHA BARAZA HILO/>BOFYA HAPA 
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania