CURRENT NEWS

Tuesday, July 4, 2017

MGALU-AMEANZISHA PROGRAM YA MWANAMKE KILIMO NA KUGAWA MBEGU ILI KUMKOMBOA MWANAMKE

Tokeo la picha la mgalu pictures
Mbunge wa viti maalum Mkoani Pwani ,Subira Mgalu 

Na Mwamvua Mwinyi ,Pwani

MBUNGE wa viti maalum Mkoani Pwani ,Subira Mgalu ,ameanzisha program ya mwanamke kilimo na kugawa mbegu mbalimbali ikiwemo za mhogo na korosho pamoja na kuanzisha shamba lake darasa la kilimo cha matunda .

Aidha mbunge huyo ,amewezesha kiasi cha sh.mil 15 kwa vikundi ndani ya jamii na kuvipatia elimu kupitia taasisi za kifedha ikiwemo bank ya wanawake Tanzania .

Hata hivyo ,Subira ,amejielekeza kuvisapoti kirahisi vikundi vitakavyounda shirikisho ama Sacco's kiwilaya katika Mkoa huo .

Mipango hiyo, aliisema wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na namna alivyoweza kusaidia makundi mbalimbali ,ndani ya mwaka mmoja uliopita na alivyojipanga kuyainua kipindi kijacho .

Subira alibainisha kwamba ,ameshaingia ushirika na taasisi ya utafiti ya Chambezi iliyopo Bagamoyo na kituo cha utafiti cha Kibaha .

Alifafanua ,amefikia hatua hiyo ,kufuatia kuona fursa ya viwanda ili kuzalisha malighafi zitakazotumika viwandani .

"Bila ya sisi wawakilishi wa wananchi kujikita kuinua kilimo na kuhamasisha kuzalisha malighafi za viwandani ili kujiinua kimaisha basi hakuna atakaeona inafaa "

"Ni wajibu wangu kuvihamasisha vikundi vya ujasirimali ,kutumia viwanda hasa vya kusindika matunda ,tutabakia kuimba Pwani ya viwanda huku tukiwa hatufaidiki navyo wazawa ." alisema Subira .

Subira alisema ,katika program hiyo ,ameahidi kupeleka mbegu za mhogo na korosho katika kikundi cha vijana cha Mwetemo na ataendelea na zoezi hilo.

Yeye akiwa ni diwani kwenye halmashauri ya Chalinze hivyo ana hakikisha anasimamia fedha za vijana na wanawake ili kuinua vipato vyao .

Kwa mujibu wake ,Chalinze ina vikundi vya wanawake zaidi ya 1,000 lakini vingi vipo kama vikoba ambapo vikipata mikopo hutumia tofauti badala ya kuzalisha .

Subira Mgalu ,alisema ,kwa kushirikiana na halmashauri watafanya utaratibu wa kuvitembelea vikundi vinavyopatiwa mikopo kujua wanavyojishughulisha .

Kwa upande wa baadhi ya akinamama Chalinze ,walisema wanashindwa kurejesha kwa wakati mikopo ya halmashauri kutokana na kutakiwa kurejesha kila mwezi .

Walisema,maisha yamebana kwa sasa ,biashara zao hazitoki kama kipindi cha nyuma .

Zubeda Hassan alisema ,anaamua kukopa kupitia taasisi nyingine za kifedha zinazowafuata vijijini kwasababu wanarejesha mikopo ndani ya miezi mitatu hadi sita .

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania