CURRENT NEWS

Friday, July 21, 2017

RPC SHANA-MAGARI MATATU YAGONGANA MMOJA AFARIKI/WAHAMIAJI HARAMU 44 WAKAMATWA PWANI


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa kisha kusababisha uharibifu baada ya magari matatu kugongana,eneo la Pichandege Kibaha mkoani Pwani,barabara kuu ya Dar –es salaam- Morogoro.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani,kamishna msaidizi wa polisi(ACP) Jonathan Shana,alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo usiku wa kuamkia july 21 .


Alisema, gari namba T.744 BBU aina ya scania likiendeshwa na dereva asiyefahamika  liligonga gari namba T.678 BRD/T.293BVA aina ya scania lililokuwa likiendeshwa na Samwel Mainya (40) mkazi wa mkoa wa Mbeya,; Pamoja na gari lenye namba za usajili T.188 ANV aina ya scania lililokuwa likiendeshwa na Hashimu Mhina (36) mkazi wa Dar es Salaam.

Kamanda Shana ,alieleza , mtu mmoja asiyefahamika alifariki papo hapo huku dereva wa gari namba T.678 BRD/T.293 BVA alijeruhiwa.

Alisema chanzo cha ajali hiyo kimetokana na dereva wa gari namba T.744 BBU kuyapita magari mengine pasipo kuchukua tahadhari na dereva wa gari hiyo alikimbia baada ya kusababisha ajali .

Kamanda Shana ,alimtaka dereva wa gari hiyo kujisalimisha mara moja ndani ya siku tatu na iwapo atashindwa kufanya hivyo jeshi hilo litamsaka kwa nguvu zao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.

Majeruhi amelazwa katika Hospitali Teule ya Tumbi akipatiwa matibabu na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo ukisubiri kukabidhiwa ndugu kwa mazishi.

WAKATI HUO HUO jeshi la polisi mkoani humo linawashikilia raia 44 kutoka nchi ya Ethiopia kwa kosa la kuingia nchi bila ya kibali.

Kamanda Shana alifafanua kuwa, raia hao walikamatwa huko eneo la Lazaba kata ya Makurunge tarafa ya Mwambao,wilaya ya Bagamoyo wakiwa wametelekezwa porini kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Kufuatia tukio hilo, jeshi la Polisi mkoa wa Pwani linafanya uchunguzi wa kina kuweza kubaini wale waliowasaidia kuingia nchi wahamiaji haramu hao, njia waliyotumia kuingia nchini, usafiri walioutumia, wafadhili wao na watu waliowatelekeza kwa lengo kujibu tuhuma hizo zinatakazokuwa zinawakabili.

“Tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria wale wote wanaohusika kushiriki kufanya biashara ya kusafirisha wahamiaji hao ndani ya mkoa na nchi hii kupitia lango la mkoa huu kwa kuwachukulia hatua”alisema.

Kamanda Shana ,alibainisha kwamba,watuhumiwa wahamiaji hao watawakabidhi idara ya uhamiaji kwa hatua nyingine zinazostahiki.

Katika hatua nyingine,alitaka ushirikiano kwa askari wa jeshi hilo mkoani hapa na wananchi baada ya kuchukua nafasi ya kamishna msaidizi mwandamizi, Onesmo Lyanga aliyehamishiwa mkoa wa kipolisi Rufiji ambao utakuwa na wilaya za Rufiji, Mkuranga, Kibiti na Mafia .


“Baada ya kugawanyika kwenye utoaji wa huduma za Kipolisi na sisi Mkoa wa Pwani kubaki na Wilaya za Kipolisi Chalinze na Mlandizi, na Wilaya za Kiserikali Bagamoyo, Kisarawe, na Kibaha”alisema kamanda Shana.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania