CURRENT NEWS

Sunday, August 6, 2017

BONDIA IBRAHIM MGENDA APONGEZWA KWA KUPATA MKANDA
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe leo jioni tarehe 6 Agosti, 2017 amekuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kumpongeza bondia mtanzania Ibrahim Class Mgenda aliyepata mkanda wa "World Championship Light Weight" baada ya kumshinda bondia aliyekuwa akitetea mkanda huo, Joseph Arero  kutoka nchi ya Panama tarehe 1 Julai, 2017 nchini Ujerumani. 

Akimkaribisha Waziri Mwakyembe, Rais wa Kamisheni ya Ngumi za kulipwa nchini Bw. Chaulembo Palasa alimshukuru kwa kujumuika nao na kumhakikishia utendaji unaozingatia weledi na sheria kwa manufaa ya mabondia na Taifa kwa ujumla.

 Waziri Mwakyembe akihutubia adhira hiyo alimpongeza bondia Ibrahim kwa kufanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya taifa na kushinda kwenye pambano hilo la kimataifa lililoandaliwa na Global Boxing Council. 

Waziri Mwakyembe pia aliviasa vyama vyote vinavyojihusisha na mchezo wa ngumi kuzingatia Sheria za nchini na kujisajili kabla ya kuanza kujihushisha na mchezo huo. "Hatutavumilia tena mapromota na vyama ambavyo havijasajiliwa na BMT na vinavyoshusha umahiri wa mabondia wetu kwa kuwarubuni wakubali kupigwa kwa kulipwa fedha ndogo ili kuwainua mabondia wa nchi za nje" alisisitiza Waziri Mwakyembe. 

Kwa upande wake, Ibrahim alimshukuru Waziri Mwakyembe kwa kushiriki kwenye hafla hiyo na kuweka wazi msimamo wa Serikali katika kuendelea kuusimamia mchezo wa ngumi.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania