CURRENT NEWS

Friday, August 25, 2017

JAFO AWATAKA WATAALAM WA LISHE KUFIKISHA ELIMU YA LISHE KWA JAMII.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza katika mkutano wa urutubishaji vyakula. Baadhi ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo.
.........................................................................
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi Mhe. Selemani Jafo amewataka wataalam wa lishe nchini kufikisha elimu ya lishe kwa jamii kwa lugha nyepesi ya kiswahili katika jamii.

Jafo aliyasema hayo wakati wa ufungaji wa mkutano mkuu wa siku mbili wa wataalam wa mambo ya lishe uliokuwa ukilenga suala la urutubishaji wa vyakula hapa nchini.

Mkutano huo wa kitaifa ulifanyikia Dar as salaam katika ukumbi wa kimataifa wa Nyerere ambapo wataalam wa lishe, watafiti, wadau wa maendeleo, wamiliki wa Viwanda vya kurutubisha vyakula, pamoja na wananchi walishiriki.

Akizungumza katika mkutano huo, Jafo alitoa angalizo kwa wataalam na watendaji kutumia lugha isiyo rafiki kwa wananchi (lugha ya kiingereza) wakati wa kujadili na kufikisha elimu ya lishe.

Jafo amesisitiza matumizi ya lugha ya kiswahili ili wananchi walengwa wa elimu hiyo waweze kufahamu nini kinajadiliwa na namna ya utekelezaji wake ili kufanikisha mapambano dhidi ya tatizo la utapiamlo hapa nchini.

Aidha, Jafo amezitaka taasisi zinazosimamia ubora wa vyakula TBS na TFDA kuongeza ufanisi wa usimamizi wa bidhaa ili viwanda vinavyorutubisha vyakula vitekeleze wajibu wao na wasisite kuwachukulia hatua wale wote wataokiuka utaratibu.

Amesisitiza urutubishaji wa chumvi kwa kuweka madini joto sambamba na urutubishaji wa unga wa mahindi, ngano na mafuta ya kula.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania