CURRENT NEWS

Wednesday, August 2, 2017

JESHI LA POLISI PWANI LAWASHIKILIA 11 KWA UUZAJI/KUTUMIA BANGI-RPC SHANNA


Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

JESHI la polisi mkoani Pwani ,linawashikilia watu kumi na moja(11), kwa kosa la kutumia na uuzaji wa baadhi ya madawa ya kulevya ikiwemo bangi kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Watu hao wamekamatwa kufuatia doria inayoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani humo,ikiwa sasa ni siku ya saba tangu kuanza kwa zoezi hilo .

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Pwani ,kamishna msaidizi wa polisi (ACP) Jonathan Shanna ,watuhumiwa walikutwa na jumla ya kete 118 na gram tatu .

Katika hatua nyingine ,alieleza mnamo july 31 huko Changwahela kata ya Mapinga ,Bagamoyo ,askari waliopo kwenye msako walipata mali zidhaniwazo ni za wizi .

"Wakiwa kwenye doria walikamata watu wanne na pikpiki moja aina ya fekon yenye namba za usajili MC.723 AMW ,spana za kufungulia bidhaa za pikipiki za aina mbalimbali na koti moja ambalo ni sare ya JWTZ " alisema kamanda Shanna.

Kamanda Shanna, alibainisha kuwa huko Mlandizi wilaya ya kipolisi Mlandizi ilitokea ajali na kusababisha kifo.

Alisema gari yenye namba T.558.CFY aina ya Vits ikiendeshwa na Saidi Yusuph (58) mkazi wa Buguruni akitokea Miswe kwenda Mlandizi alimgonga mwendesha pikipiki Steven Charles (18)mkazi wa Mlandizi aliyekuwa akitokea Mlandizi kwenda Mlandizi Bondeni na kusababisha kifo chake papohapo.

Kamanda huyo ,aliweka wazi kuwa ,misako inayofanywa ni endelevu kwa lengo la kuweka mkoa katika hali ya usalama.

Aliwaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwafichua wahalifu waliopo katika maeneo yao .

Wakati huo huo ,kamanda Shanna aliwataka madereva na watuamiaji wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabara ili kuepukana na ajali za barabarani .

Jeshi hilo limeendelea kusisitiza kwamba halitakuwa na muhali pindi watakapowakamata watu wote wanaovunja sheria za nchi zilizopo .

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania